Tuesday, June 24, 2014

WATANZANIA WASHAURIWA KUANDIKA WOSIA ILI KUEPUSHA MIGOGORO BAADA YA KIFO


Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Mwanza Mh. Aishiel Sumari amewataka wananchi kujenga tabia ya kuandika wosia ili kulinda haki ya warithi baada ya kifo, jambo ambalo litasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza migogoro ya kugombea mali na maiti, sanjari na kuwalinda watoto wa nje ya ndoa ambao kisheria hawapaswi kurithi mali iliyoachwa na marehemu.

Jaji huyo mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Mwanza ametoa changamoto  hiyo jijini Mwanza wakati akifungua kongamano lililoandaliwa na shirika la msaada wa sheria Mwanza, lenye maudhui yasemayo, ‘ linda haki za uwapendao, andika wosia ambapo amesema katika jamii nyingi duniani, wosia ni kitu kinachotambulika kutokana na kuwa na nguvu za kisheria ambapo kwa hapa nchini sheria za mirathi zinatambua kuwepo kwa wosia, ulioandaliwa na mwenye kumiliki mali wakati akiwa bado yu hai na vilevile akili zake zikiwa bado timamu.

Mapema mkurugenzi  mtendaji wa shirika la msaada wa sheria Mwanza Bw. Heri Emanuel amesema kwa hali ya kawaida mtu akifariki bila kuacha wosia sheria inalazimu vikao vya wanandugu kuketi na kuteua msimamizi wa mirathi, jambo ambalo wakati mwingine linaweza kusababisha kutoelewana huku gharama kubwa zikitumika katika uratibu na uendeshaji wa vikao hivyo kama chakula, vinywaji na mifugo aliyoacha marehemu badala ya kutumika kwa mustakabali wa warithi wa marehemu.

Mtu anapofariki bila ya kuacha wosia, waathirika wakubwa ni wajane pamoja na watoto walioachwa na marehemu ambapo matokeo yake ni kunyimwa haki ya kurithi, kudhulumiwa au kudhulumiana kati ya warithi na kwa hali hiyo wananchi wanapaswa kuachana na dhana potofu kwamba kuandika wosia ni uchuro na njia pekee ya kuepusha migongano ya aina hiyo ni mtu kuandika wosia kuliko ule wa kutoa kwa mdomo.

0 Responses to “WATANZANIA WASHAURIWA KUANDIKA WOSIA ILI KUEPUSHA MIGOGORO BAADA YA KIFO ”

Post a Comment

More to Read