Monday, June 30, 2014
WAZIRI MKUU: MAANDALIZI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA YANAENDELEA
Do you like this story?
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema maandalizi ya
uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao unatarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu
yanaendelea japo kwa kiasi kikubwa hatma yake inategemea kukamilika kwa
mchakato wa Katiba mpya.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Jumatatu, Juni 30,
2014) wakati akizungumza na Mameya wa Majiji, Manispaa na Wenyeviti wa
Halmashauri za Miji na Wilaya Tanzania katika kikao cha siku moja
kilichofanyika kwenye ukumbi wa Regal Naivera jijini Tanga.
Waziri Mkuu yuko Tanga kwa ajili ya sherehe za
Serikali za Mitaa ambayo kilele chake kitafanyika kesho Julai mosi kwenye
uwanja wa Tangamano jijini hapa. Ameamua kukutana na viongozi hao ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi ya kukutana nao aliyoitoa Mei 14, 2014 wakati akifungua
Mkutano Mkuu wa ALAT.
“Uchaguzi wa Serikali za Mitaa bado ni kitendawili
kwa sababu kwa kiasi kikubwa inategemea sana kukamilika kwa Mchakato wa Bunge
la Katiba,” alisema na kuongeza:
“Kama Wizara tunaendelea na maandalizi tukiamini
uchaguzi upo, kama hiyo fursa isipotokea bado tutakuwa tumekamilisha maandalizi
kwa upande wetu.Tunaendelea kuandaa kanuni kwa kushirikisha wadau wote,”
alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kusisitiza suala la
ukusanyaji mapato na udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali. Kuhusu mapato,
Waziri Mkuu alisema katika mwaka wa fedha wa unaoisha sasa, hali ya ukusanyaji
mapato haikuwa nzuri.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Mkuu alisema amewaandikia
barua Wakuu wa Mikoa akiwataka waweke utaratibu wa kutoa taarifa kila baada ya
miezi mitatu juu ya makusanyo ya kila Halmashauri zilizo kwenye mikoa yao.
“Katika taarifa hizi itabidi kila Halmashauri ieleze
ilipanga kukusanya kiasi gani, je imefikia lengo na kama sivyo ni kwa nini. Nia
yetu ni kutrack down makusanyo na kuona yamekwama wapi na yamekwamishwa na
nini,” alisema.
Kuhusu udhibiti wa matumizi, Waziri Mkuu aliwataka
Mameya na Wenyeviti hao kuendelea kuwabana wahusika ili kudhibiti matumizi
yasiyofaa. “Lazima muendelee kuwabana na kuwasimamia wakurugenzi na wataalaam wa
kwenye Halmashauri zenu. Fanyeni kazi kwa ufanisi, msiwachekee wale
wanaoharibu,” aliongeza.
“Ili muweze kuwabana vizuri, ni lazima mdai kupatiwa
taarifa za fedha kutoka kwa Mkaguzi wa Ndani (Internal Auditor)… kuna baadhi ya
watendaji wanadai kuwa hizi taarifa ni siri wakati siyo siri,” alisema.
Aliwaeleza washiriki wa kikao hicho kwamba taarifa
hizo ni muhimu kwao kuzipata na zitawasaidia kuonyesha mapungufu yoyote kama
yapo.
Aliwataka kila mmoja wao kwa nafasi zao za Meya na
Mwenyekiti wahakikishe wanalenga kupandisha pato la wananchi wanaowaongoza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MKUU: MAANDALIZI YA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA YANAENDELEA”
Post a Comment