Wednesday, July 2, 2014

ASILIMIA 47 WANAUME JIJINI DAR ES SALAAM NI WALEVI,WANAWAKE 29%



KATIKA kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana unaosababishwa na ulevi wa pombe, Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa) kupitia Kituo cha Usuluhishi (CRC), kimezindua mradi wa kupambana na kupunguza ulevi huo.

Akitambulisha mradi huo kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini, Mkurugenzi Mtendaji wa Tamwa, Valeria Msoka, alisema kuwa unafadhiliwa na Shirika la IOGT International la Sweden.

Msoka alisema kuwa kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2010, uliofanywa na shirika hilo, ulionyesha kwamba kiwango cha unywaji pombe katika Jiji la Dar es Salaam ni asilimia 47.6 kwa wanaume na asilimia 29 kwa wanawake.
“Malengo ya mradi huu ni kuboresha maisha ya wanawake na watoto kwa kuimarisha sheria na kupunguza ukatili wa kijinsia unaosababishwa na unywaji wa pombe katika Wilaya ya Kinondoni.


“Pia tunataka kujenga uelewa miongoni mwa jamii juu ya madhara yanayotokana na unywaji wa pombe kwa kutumia takwimu za wilaya hii kama sehemu ya wilaya zote nchini kwa kuanzia,” alisema.

Kwa mujibu wa Msoka, wanalenga kujengea uwezo jamii kukabiliana na ukatili unaosababishwa na unywaji pombe dhidi ya wanawake na watoto na kutoa msaada wa kisheria kwa waathirika.

“Wanawake ambao waume zao wanalewa mara kwa mara, wengi wao wanakumbana na ukatili unaohusisha kipigo/kuumizwa na ukatili wa kingono kwa asilimia 77.
“Kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake ambao waume/wenzi wao hawanywi pombe ni asilimia 33,” alisema.
Aliongeza kuwa utafiti uliofanywa na IOGT mwaka 2012, katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Iringa ulionyesha kuwa asilimia 58.3 ya watu
waliohojiwa walikubali kuwa kuna wazazi walishindwa kuwapeleka watoto wao shule kwa sababu ya ulevi.

Kwa mujibu wa Msoka, mradi huo utatekelezwa katika Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo utadumu kwa miaka mitatu; 2014-2016.


Alisema kuwa kazi za mradi ni kufanya utafiti wa awali juu ya kiwango cha matumizi ya pombe na unyanyasaji katika wilaya hiyo, na kwamba utafiti huo tayari unaendelea kupitia waandishi wa habari kwa kushirikiana na waelekezi.
via>>Tanzania daima

0 Responses to “ ASILIMIA 47 WANAUME JIJINI DAR ES SALAAM NI WALEVI,WANAWAKE 29%”

Post a Comment

More to Read