Thursday, July 3, 2014

AZAM FC KUIMARISHA MAWINDO YAKE NJE YA NCHI, OMOG KAZI KWAKE KUCHAGUA


Wanalambalamba, Azam fc watahimili kasi ya Yanga, Simba na Mbeya City ili kutetea ubingwa wao msimu ujao?



MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc wanatarajia kuweka kambi nje ya nchi kwa lengo la kujiimarisha zaidi kabla ya kuanza harakati za kutetea ubingwa wao pamoja na kucheza ligi ya mabingwa barani Afrika mwakani.

Jemedari Said, meneja wa Azam fc amesema wamepokea mialiko kadha wa kadha, lakini wanasubiri kocha mkuu,  Mcameroon, Joseph Marius Omog achague wapi atakwenda.

“Ratiba ya kwenda nje ya nchi ipo. Kuna mialiko kadha wa kadha. Mwalimu baada ya kufanya maandalizi ya hapa nyumbani, yeye ndiye atachagua wapi pa kwenda. Yeye atachagua ni wapi anaona akienda timu itafanya maandalizi mazuri na kushiriki vizuri katika michuano ya CAF na ligi kuu”. Alisema Jemeadari.

Jemedari aliongeza kuwa walipozungumza na mwalimu alisema hatapeleka timu sehemu yoyote kwa ajili ya kujifurahisha bali atapeleka timu ambapo itapata uzoefu wa ligi ya mabingwa na itakuwa ni faida pia kwa ligi ya nyumbani.

Meneja huyo alisema kama mwalimu wao ataamua kuipeleka timu sehemu ilipokuwa msimu uliopita na kutwaa ubingwa kwa maana ya Afrika kusini hilo ni juu yake na kama ataamua kwenda sehemu nyingine, pia ni maamuzi yake.

Hata hivyo kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Azam wanatarajia kuweka kambi nchini Kenya au Amerika, lakini uongozi haujasema lolote zaidi ya kumsubiri Omog achague sehemu ya kuweka chimbo lake.
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam.

0 Responses to “AZAM FC KUIMARISHA MAWINDO YAKE NJE YA NCHI, OMOG KAZI KWAKE KUCHAGUA”

Post a Comment

More to Read