Tuesday, July 8, 2014
BOMU LINGINE LALIPUKA JIJINI ARUSHA LAJERUHI WAWILI
Do you like this story?
Sheikh wa Msikiti wa Qiblatan,Sood Ally Sood
(37) uliopo Kilombero jijini Arusha amejeruhiwa kwa bomu la kurushwa kwa mkono
alipokuwa akila daku nyumbani usiku wa kuamkia jana.
Pamoja na Sheikh Sood, mtu mwingine
aliyekuwa nyumbani kwake,aliyetajwa kwa jina la Muhaji Kifea (38) mkazi wa Sinza
jijini Dar es Salaam pia amejeruhiwa katika tukio hilo na wote wamelazwa katika
Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa matibabu.
Sheikh alijeruhiwa miguu yake yote na
mapajani huku Kifea akipata majeraha makubwa miguuni na kupoteza baadhi ya
vidole vya miguu yote.
Akizungumza hospitalini hapo, Sheikh, Sood
alisema tukio hilo lilitokea nyumbani kwake eneo la Majengo ya chini, usiku wa
kuamkia jana saa 5:00 wakati yeye pamoja na mgeni wake walikuwa wakila chakula
sebuleni.
“Nikiwa sijui hili wala lile nilishtushwa na
mlipuko ulioambatana na vyuma mbalimbali vilivyokuwa vikiruka hewani ambapo
bomu hilo linaelezwa kuwa ni guruneti lililorushwa kupitia dirishani baada ya
watu wasiofahamika kufanikiwa kuvunja kioo cha dirisha la chumba
tulichokuwamo,” alisema Sheikh Sood.
Alidai anawajua waliotekeleza shambulio hilo
kwa sababu amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu anaowafahamu na tayari
alikuwa ametoa taarifa kwa vyombo vya dola.
Alisema kuwa siku tatu kabla ya tukio hilo
alikoswakoswa kupigwa risasi na watu wasiofahamika wakati akitoka msikitini na
akatoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Arusha kuhusu tukio hilo. Sood
anasema kuna baadhi ya vijana anawatuhumu juu ya matukio hayo.
Sheikh huyo ambaye ni Kiongozi wa dhehebu la
Answar sun Kanda ya Kaskazini amekuwa akitofautiana na waumini wenzake kutokana
na msimamo wake wa kutokukubaliana na baadhi ya waumini wenye msimamo mkali wa
msikiti huo.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo
alikemea matukio ya mabomu yanayolitikisa Jiji la Arusha katika siku za
karibuni na kuviagiza vyombo dola kufanya uchunguzi wa kina kubaini wahusika
wote ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
“Uchunguzi wa awali unaonyesha tukio hili
limetekelezwa na watu walio karibu na Sheikh. Polisi wanaendelea na uchunguzi
kwa sababu baadhi ya watu wanaotajwa kuhusika kwenye tukio hili pia ni miongoni
mwa watuhumiwa kwenye matukio mengine ya milipuko ya bomu Arusha,” alisema
Mulongo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatusi
Sabasi alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa majeruhi
wanaendelea vyema huku polisi wakiendelea na uchunguzi wa kina kuwabaini
wahusika.
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema
alielezea kusikitishwa na matukio ya milipuko ya mabomu Arusha na kuliomba
jeshi la polisi kufanya uchunguzi wa kina kuwakamata wahusika bila kujali vyeo,
nyadhifa, dini, itikadi wala rangi zao. Kinyaiyas Blog inajiuliza haya mambo ya
kulipuana kila kukicha na haswa mkoani Arusha yataisha lini wkt nchi yetu na
watu wake hatujazoea hayo mambo jamanii...
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “BOMU LINGINE LALIPUKA JIJINI ARUSHA LAJERUHI WAWILI ”
Post a Comment