Friday, July 25, 2014
MAGUMASHI: KABURU AZURULA NA SAADY KIPANGA WA MBEYA CITY KWENYE GARI YAKE AKISHINIKIZA ASAJILIWE..YAJIRUDIA YA ABDALLAH JUMA, PAUL NGALEMA
Do you like this story?
Makamu wa Rais wa Simba sc, Geofrey Nyange 'Kaburu' |
Mshambuliaji wa Mbeya City fc, Saady Kipanga |
MAGUMASHI yameendelea kutawala katika
usajili wa soka la Bongo ambapo viongozi wanazidi kujifanyia mambo kwa mahaba
yao.
Taarifa za uhakika ambazo mtandao huu
umezipata ni kwamba mshambuliaji hatari wa Mbeya City fc, Saady Kipanga
anazurula jijini Dar es salaam na makamu wa Rais wa Simba, Geofrey Nyange
Kaburu ikishinikiza asajiliwe.
Kamati ya usajili ya Simba chini ya
mwenyekiti wake, Zacharia Hans Poppe haimhitaji Kipanga, badala yake inamtaka
mshambuliaji wa Ruvu Shooting ya Pwani, Elias Maguri, lakini Kaburu
analazimisha asajiliwe Kipanga.
Kwasababu Kaburu ni makamu wa Rais
anaweza kuwa na nguvu ya kumsajili Kipanga, lakini mwisho wa siku sio mahitaji
ya timu na atakuwa amefanya hivyo kwa matakwa binafsi na mahaba yake.
Kaburu aliwahi kufanya jambo hili tena
katika usajili wa Abdallah Juma na Paul Ngalema kutoka JKT Ruvu. Wachezaji hawa
hawakuwepo katika mahitaji ya timu, lakini Kaburu akawasajili na wakaendelea
kukaa benchi mpaka wakatimka zao na kujiunga na Mtibwa Sugar.
Kitendo kama hicho kinajirudia tena
ambapo Kipanga anataka kuingia katika majanga hayo ya kurubuniwa na kwakuwa
anatamaa, atahitaji kupata hela za haraka, lakini nafasi ya kucheza itakuwa
finyu.
Kama kweli anataka kusajiliwa kwa
`staili` ya magumashi kiasi hicho, bila kujali uhitaji wa timu, ataishia
kuharibu kipaji chake
MAGUMASHI YAKO WAPI KATIKA SUALA HILI?
Saady Kipanga ni mchezaji wa Mbeya
City fc. Alisajiliwa mwezi desemba mwaka jana kutokea klabu ya Rhino
Rangers na kupewa mkataba wa miaka miwili.
Kwasasa amebakiza mwaka mmoja wa
kuitumikia Mbeya City fc. Kiutaratibu ni mchezaji halali wa Mbeya City na kama
klabu inamhitaji, hakuna jinsi, lazima wafike Mbeya kuzungumza biashara.
Kipanga si mchezaji huru. Yupo
mapumziko baada ya Mbeya City fc kuamua kuvunja kambi kutokana na shirikisho la
soka Tanzania kusogeza mbele ligi kuu mpaka septemba 20 mwaka huu.
Kaburu anafanya mambo kizamani
kwasababu Simba na Yanga zimezoea kusajili kinyume na taratibu. Duniani kote,
timu haiwezi kuongea na mchezaji binafsi bila kuishirikisha timu yenye mkataba
naye.
Biashara ya Kipanga inaweza kufanyika
baina ya klabu ya Mbeya City fc na Simba, lakini si Kaburu na Kipanga. Huu ni
`upuuzi` usiotakiwa tena wakati huu Tanzania inahangaika kujinasua katika
magumashi ya soka.
Kaburu ni mtu wa mpira na bila shaka
anajua kanuni na taratibu za usajili, kwanini ashindwe kuheshimu mkataba wa
mtu?
Halafu kwanini atake kumsajili yeye?
Kaburu ni kocha?, au ni mjumbe wa kamati ya usajili?
Kiutaratibu, kocha mkuu ndiye
anayependekeza wachezaji wa kuwasajili na kupeleka majina kwenye kamati ya
usajili.
Leo hii Kaburu anataka kumsajili
Kipanga wakati jina la mchezaji lililopo mezani ni Elias Maguri. Kamati ya
usajili inamtaka Maguri, kwanini Kaburu ashinikize kusajiliwa kwa Kipanga, kuna
nini nyuma ya pazia”
KUTOJITAMBUA KWA SAADY KIPANGA
Kipanga ni miongoni mwa wachezaji
waliokosa ueledi kabisa. Kwanini anashindwa kuheshimu mkataba? Yeye ni mchezaji
wa Mbeya City fc.
Kwa maana hiyo kama timu au kiongozi
yoyote anamfuata na kuzungumza naye ili amsajili, lazima awaelekeze kwa
viongozi wa Mbeya City kwasababu wao ndio wana haki zote.
Kuzurula na kaburu hapa mjini badala ya
kuwasiliana na viongozi kama anataka kuichezea Simba ni kukosa elimu tu. Haya
ndio matatizo ya wachezaji wa Tanzania.
SOMO KWA KIPANGA
Abdallah Juma na Paul Ngalema walikuwa
wachezaji wazuri, lakini walirubuniwa na Kaburu na kusajiliwa Simba. Kiukweli
hawakuhitajika na klabu. Wakaishia kukaa benchi na kuua vipaji vyao mpaka
wakaamua kuondoka.
Kipanga naye anaingia katika mkumbo
huo. Itamgharimu na kipaji chake kitaishia hapo asipojiangalia.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAGUMASHI: KABURU AZURULA NA SAADY KIPANGA WA MBEYA CITY KWENYE GARI YAKE AKISHINIKIZA ASAJILIWE..YAJIRUDIA YA ABDALLAH JUMA, PAUL NGALEMA ”
Post a Comment