Monday, July 21, 2014
MAMBO YAPAMBA MOTO ZIARA YA MAGWIJI WA REAL MADRID NCHINI.
Do you like this story?
WAZEE wa kale walishasema, `Bahati
haiji mara mbili`!. Kumekucha kwa Watanzania kuwaona `laivu` magwiji
waliotikisha soka la dunia ngazi ya klabu na michuano ya kimataifa ikiwemo
kombe la dunia.
Magwiji waliocheza kwa mafanikio
makubwa katika klabu ya Real Madrid wanatarajia kufanya ziara ya siku nne
nchini kuanzia Agosti 22 mwaka huu ambapo watacheza mechi moja ya kirafiki
dhidi ya kikosi maalum cha nyota wa Tanzania.
Ziara hiyo ni mwaliko wa kampuni ya
Tanzania Sisi ni Nyumbani (TSN), chini ya mkurugenzi wake mkuu, Farough
Baghozah na meneja wa ziara hiyo ni Dennis Ssebo.
Akizungumza na mtandao huu mchana wa
leo, Dennis Ssebo amesema maandalizi ya ziara hiyo yanakwenda vizuri na
watanzania watarajie kuwaona wachezaji wakubwa waliotamba miaka ya nyuma kama
vile Ronaldo Delima, Luis Figo, Roberto Carlos, Zinedine Zidane na wengineo.
“Ninaloweza Kusema ni kwamba,
Watanzania wakae tayari kupokea wachezaji 27 wa zamani wa timu ya Real
Madrid na mashabiki 23 kutoka Hispania wanaokuja kuwashangilia magwiji
wao. Kwahiyo jumla tunapokea watu 50 kutoka Hispania kwa ajili ya ziara hii”.
Alisema Ssebo.
“Ni ziara ambayo tulifikiria itakuwa fupi,
lakini wenzetu kumbe wameipenda nchi na wanaifahamu, kwahiyo ni ziara ambayo
itachukua takribani siku nne”. Aliongeza.
Ssebo alisema Magwiji hao wataingia
nchini Agosti 22 mwaka huu na watacheza mechi maalumu ya kirafiki Agosti 23
ndani ya dimba la kisasa la Taifa, jijini Dar es salaam.
“Baada ya mechi wataenda Arusha Agosti
25 kuangalia vivutio vya utalii na watalala huko. Watalala tena Dar es salaam
na kuondoka tarehe 26 ya mwezi wa nane”.
“Kwahiyo ni ziara ambayo ni ndefu
kidogo, watu ni wengi, tulifikiri timu ingekuja peke yake, kumbe kuna mashabiki
wanaotoka Hispania kuwashangilia hao magwiji, nafakiri Watanzania tukae mkao wa
kula,”. Alifafanua Ssebo.
Kuhusu viingilio vya mechi hiyo, Ssebo
alisema watakuwa na kiwango cha chini kinachoweza kulipwa na watanzania wengi.
“Tunawahakikishia watanzania kuwa
wataangalia mechi hii kwa kiwango cha chini kabisa.”
“Naweza kuthubutu kusema kuwa kiwango
cha chini kabisa kitakuwa shilingi elfu 5 ambacho tunaamini Watanzania wa
kawaida wataipata kwasababu tumewaambia mapema kwa mwezi mzima.” Ssebo alisema.
“ Lakini kikubwa zaidi, ni
kuwahakikishia watanzania kuwa ziara hii itafungua milango ya kujiuza na kuuza
vivutio vyetu vya utalii”.
“ kwahiyo ni zaidi ya mpira na sisi
tunaamini kabisa kuwa tutakuwa na uwezo wa kuuza vitu vyetu, kwasababu wao
watakuja na mashabiki, halafu Real Madrid TV watakuja kurekodi ziara nzima timu
ikiwa Tanzania”. Alisema Ssebo.
Hii ni ziara ya kwanza kabisa kwa klabu
ya Real Madrid kufanya barani Afrika, hivyo ni bahati kwa Tanzania kuwa nchi ya
kwanza kutembelewa na timu kubwa ya Real Madrid.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAMBO YAPAMBA MOTO ZIARA YA MAGWIJI WA REAL MADRID NCHINI.”
Post a Comment