Monday, July 21, 2014

WIZARA YATOA ONYO KALI KWA UVUVI HARAMU UNAOENDELEA KATIKA BWAWA LA MWANZUGI.




Wizara ya Mifugo na Uvuvi kanda ya kati imewaagiza watu wote wanaojishughulisha na uvuvi haramu kwenye bwawa la Mwanzugi,lililopo katika Kijiji cha Mwanzugi,wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora usiofuata taratibu zilizowekwa waache mara moja na kwamba endapo wataendelea kukaidi amri hiyo halali hatua kali na za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Afisa Uvuvi Mfawidhi na uvunaji wa viumbe hai Kanda ya kati,Bwana Renatus Charles Karumbeta alisema hayo katika mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti hilo kufuatia malalamiko kwamba licha ya bwawa la Mwanzugi kufungwa lakini bado kuna baadhi ya wavuvi kwa kushirikiana na maafisa uvuvi wanaokwenda kuvua nyakati za usiku.

Aidha Bwana Karumbeta alifafanua kwamba uvuvi haramu ni kuanzia kutokuwa na leseni pamoja na kuvua samaki wadogo,hivyo kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya ya Igunga wamejipanga kuhakikisha kwamba wavuvi wote wanavua katika eneo hilo wanafuata taratibu na kwamba hawatakuwa tayari kukukabaliana kuruhusu uvuvi haramu uendelee katika wilaya hiyo.

Alifafanua afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia ufugaji samaki katika mikoa ya Dodoma,Singida na Tabora kuwa idara hiyo imeshaanza zoezi la kupandikiza samaki na kwamba mpaka sasa jumla ya vifaranga 22,000 vya samaki katika bwawa la Kijiji cha Igogo vimekwishapandikizwa.

“Kwa hiyo tunashirikiana na serikali ya Kijiji pamoja na serikali ya wilaya ya Igunga kuhakikisha kwamba samaki wale wanalindwa ili waweze kufaidisha wananchi wote wa eneo zima”alifafanua zaidi Karumbeta.

Hata hivyo afisa Mfawidhi huyo alisisitiza kwamba serikali wilayani Igunga haitakubali kikundi kidogo cha watu ambao hawataki kufuata taratibu kuharibia jamii nzima kwa sababu wanajua uvuvi au ufugaji wa samaki ni vitu ambavyo vinakwenda pamoja.

Alisema pamoja na kifaranga kimoja kuzalishwa kwa shilingi mia tatu lakini serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi imeweza kupunguza bei ili wananchi wengi waweze kununua na kila kifaranga kitauzwa kwa bei ya shilingi mia moja.

Kwa mujibu wa Bwana Karumbeta kwa kuwa wanawategemea wadau wao wakubwa kuwa ni Halmashauri za wilaya,Mji na Manispaa zilizopo katika mikoa ya Dodoma,Singida na Tabora alizishauri kuanza kuona umuhimu wa ufugaji wa samaki kwa sababu hivi sasa hakuna tatizo la mbegu lililokuwa likiwakabili hapo awali wananchi wa mikoa hiyo.

“Kituo hiki kinatarajiwa kutoa vifaranga vya samaki laki mbili kila mwezi kwa hiyo tunaomba Halmashauri,Taasisi mbali mbali na watu binafsi waje kwenye kituo hiki kujifunza namna ya ufugaji bora wa samaki”.alifafanua Bwana Karumbeta.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwanzugi,Bwana Kusweka Kaswenye alitumia fursa hiyo kuiomba wizara ya kilimo na ushirika kwa kushirikiana na serikali ya wilaya kuhakikisha wakulima wa aina hiyo wanadhibitiwa kikamilifu kwa madai kuwa uharibifu unaofanywa na wakulima hao ni mkubwa zaidi kuliko ule unaofanywa na wavuvi haramu.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanzugi,Bwana Abeli Nchimo alisema ili kukabiliana na wavuvi haramu serikali ya Kijiji hicho imejipanga kwa kutumia askari wa jeshi la jadi,”Sungusungu”kufanya doria usiku na mchana katika bwawa hilo.

0 Responses to “WIZARA YATOA ONYO KALI KWA UVUVI HARAMU UNAOENDELEA KATIKA BWAWA LA MWANZUGI.”

Post a Comment

More to Read