Thursday, July 31, 2014
RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA AJALI MBAYA YA BASI LA MORO BEST.
Do you like this story?
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais Jakaya Mrisho Kikwete
amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Rehema Nchimbi
kufuatia ajali iliyotokea tarehe 30 Julai, 2014 katika eneo la Pandambili,
Wilayani Kongwa na kuua watu wapatao 18.
Katika ajali hiyo, watu 13
walifariki katika eneo la ajali, na majeruhi wapatao 56 walifikishwa
hospitalini. Kati ya majeruhi hao hadi sasa waliolazwa ni 30 na wengine
wameruhusiwa baada ya kupata matibabu.
Rais amemuomba Dkt. Nchimbi
kumfikishia rambirambi zake za dhati kwa ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa
wao katika ajali hiyo, na kuwapa pole majeruhi wote na kuwatakia kupona haraka
ili warejee kwenye shughuli zao za kila siku.
“ Natoa Pole za dhati kwa wale
wote walioondokewa na wapendwa wao katika ajali hii na pia kuchukua nafasi hii
kuwapa pole majeruhi wote na kuwaombea kupona haraka na kurudi katika shughuli
zao za kila siku”. Rais amesema katika salamu zake kwa Mkuu wa Mkoa
wa Dodoma.
“Hakika ni jambo la kusikitisha
sana kuondokewa na wananchi wetu katika ajali , natoa wito wangu kwa madereva
wote na wote wanaotumia vyombo vya moto kuwa makini wanapokuwa barabarani
“. Rais amesema na kuongeza kuwa;
“Kila dereva anaetumia chombo cha
moto, ana wajibu wa kulinda maisha yake na ya watumiaji wengine kwa
kuwa makini na muangalifu awapo barabarani, kwani ajali hizi zinarudisha nyuma
maendeleo ya taifa na ya wananchi kwa ujumla” Rais amesema
na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama barabarani kutolegeza kamba
katika kuwachukulia hatua madereva wasio makini na wazembe wakati wote”.Rais amesisitiza.
Taarifa kutoka Mkoani Dodoma
zinasema ajali hiyo ya jana (30 Julai, 2014) ilisababishwa na
Lori ambalo lilitaka kupita lori jingine na hivyo kwenda kugongana
uso kwa uso na Basi la Moro Best lililokuwa likitokea Mpwapwa kuelekea Dar es
Salaam.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais
Msaidizi,
Ikulu – Dar es Salaam.
30 Julai, 2014
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ RAIS KIKWETE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA AJALI MBAYA YA BASI LA MORO BEST.”
Post a Comment