Thursday, July 10, 2014
SITTA ATEUA MASHEIKH,MAASKOFU KUWAREJESHA UKAWA BUNGENI.
Do you like this story?
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta ameanza mkakati mpya wa kunusuru mchakato wa Katiba Mpya kwa kuitisha kikao cha wajumbe 27 wa Kamati ya Mashauriano ili kuondoa mpasuko kati ya wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na wajumbe wengine.
Katika
wajumbe hao wamo maaskofu wawili na masheikh wawili ambao Sitta amewateua
kutoka katika Bunge la Katiba.
Sitta
ameitisha kikao hicho jijini Dar es Salaam Julai 24 wakati kukiwa na matamko
tofauti kuhusu mustakabali wa katiba hiyo, mengi yakieleza kuwa Rais Jakaya
Kikwete ndiye aliyeshikilia hatima ya mchakato na wapinzani wakisema mkuu huyo
wa nchi ndiye aliyesababisha suala hilo kwenda mrama.
Pia,
Sitta ameitisha kikao hicho wakati viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
wakieleza kuwa suala la serikali mbili kwenye muundo wa Muungano, ambalo
liligawanya wajumbe, ndiyo msimamo wa chama na wapinzani wakisema suala hilo
halimo kwenye Rasimu ya Katiba na ndiyo sharti lao la kurejea bungeni.
Akizungumza
jana katika mahojiano na gazeti hili, Sitta alisema miongoni mwa mambo
yatakayojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja kutazama mwenendo wa majadiliano
katika Bunge hilo na sura 15 za katiba ili kujua yapi muhimu yanayotakiwa
kupewa kipaumbele kabla ya Bunge la Katiba kuanza tena vikao vyake Agosti 5.
“Sisi
tumeshapeleka barua kwa wajumbe, tumehakikisha zimekwenda na katika mkutano huo
tutaelewana kuhusu masuala hayo na mengine. Wasiotaka kuhudhuria wananchi
watawaelewa na wataamua iwapo nia ni kususa pekee au wenzetu wana ajenda ya
siri,” alisema Sitta.
Alisema
katika mkutano huo, kutakuwa na utaratibu maalumu ambao utahusisha viongozi wa
dini walio ndani ya Bunge kutoka madhehebu tofauti na baadhi ya wajumbe wengine
kutoka kada tofauti ndani ya Bunge hilo.
“Kutakuwa
na watu karibu 27, mimi nikiwa mwenyekiti. Atakayevimba kichwa na kudharau,
wananchi watajua kuwa nia yake ni tofauti na katiba,”
Sitta
alisema tatizo kubwa katika Bunge hilo litakalosababishwa na kutokuwapo kwa
Ukawa ni namna ya upigaji kura, lakini iwapo theluthi mbili ya wajumbe
itatimia basi watakwenda kwa mwenendo huo.
“Yapo
mambo muhimu zaidi katika rasimu hii kama vile tume huru ya uchaguzi, orodha ya
haki za binadamu, uongozi wa asilimia 50 kwa 50 kijinsia na kuwapa Zanzibar
nafasi zaidi katika Serikali ya Muungano, mambo ambayo ni makubwa kuliko
muundo...ya nini kuyapiga teke yote haya na kujikita katika muundo pekee,”
alihoji.
Sitta
ambaye pia alipingwa kwa kumpanga Rais Kikwete kuhutubia Bunge hilo baada ya
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha
Rasimu ya Katiba tofauti na kanuni, alisema kuwa kuususia mkutano huo wa Bunge
katika kipindi chote hicho siyo hasara kwa CCM, bali kwa wananchi kwa kuwa nia
ni kupata katiba bora na wala siyo kukomoana.
“Iwapo
Ukawa watasusia kila kitu, basi wataonyesha kuwa siyo wakomavu wa kisiasa,”
alisema mbunge huyo wa Jimbo la Urambo Mashariki.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SITTA ATEUA MASHEIKH,MAASKOFU KUWAREJESHA UKAWA BUNGENI.”
Post a Comment