Tuesday, July 29, 2014
TAIFA STARS KWENDA AFRIKA KUSINI KESHO.
Do you like this story?
Msafara wa watu 27 wa kikosi cha
timu ya Taifa (Taifa Stars) kinaondoka kesho (Julai 30 mwaka huu) saa 10 jioni
kwa ndege ya Air Tanzania kwenda Afrika Kusini ambapo kitapiga kambi ya siku
mbili kabla ya kuingia Maputo kuikabili Msumbiji (Mambas).
Taifa Stars inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager itawasili saa 9 asubuhi kesho (Julai 30 mwaka huu)
kwa ndege ya Fastjet, na baadaye jioni kuunganisha safari ya Afrika Kusini.
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi
ya pili ya michuano ya Afrika dhidi ya Msumbiji itachezwa Agosti 3 mwaka huu
Uwanja wa Taifa uliopo Zimpeto nje kidogo ya Jiji la Maputo.
Msafara huo wa Taifa Stars kwenda
Afrika Kusini unajumuisha wachezaji 19 na waliobaki ni maofisa wa Benchi la
Ufundi lililo chini ya Kocha Mkuu Mart Nooij kutoka Uholanzi.
Wakati kiungo Mwinyi Kazimoto
ametua leo (Julai 29 mwaka huu) nchini kuungana na wenzake, washambuliaji
Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wao wataungana na wenzao kesho (Julai 30
mwaka huu) jijini Johannesburg wakitokea Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya
Congo (DRC).
Wakati huo huo, Serengeti Boys
imewasili salama jana (Julai 28 mwaka huu) jijini Johannesburg, Afrika Kusini
kwa ajili ya mechi ya michuano ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka
17 dhidi Afrika Kusini (Amajimbos).
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi
ya pili itachezwa Jumamosi, Agosti 2 mwaka huu kwenye Uwanja wa Dobsonville
uliopo Soweto kuanzia saa 9 kamili mchana kwa saa za Afrika Kusini.
Timu hizo zilitoka suluhu katika
mechi ya kwanza iliyofanyika Julai 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex,
Dar es Salaam. Serengeti Boys inahitaji ushindi kwenye mechi hiyo au aina
yoyote ya sare ya mabao ili ifuzu kwa raundi ya tatu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TAIFA STARS KWENDA AFRIKA KUSINI KESHO.”
Post a Comment