Monday, July 21, 2014
WAALIMU WENYE DIGRII MBIONI KUFUNDISHA SHULE ZA MSINGI.
Do you like this story?
RAIS Jakaya Kikwete amesisitiza nia ya
Serikali kutumia wahitimu wake wa vyuo vikuu, kufundisha shule za msingi huku
akiwaweka sawa kwa kuwaambia kufanya hivyo si kuwashushia hadhi.
Hatua hiyo ya walimu wenye Shahada
kuanza kufundisha shule za msingi tofauti na ilivyozoeleka, chini ya Sera ya
Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, ni sehemu ya mageuzi makubwa, yanayotarajiwa
kufanyika katika sekta ya elimu nchini.
Rais Kikwete alishawahi kutamka mpango
huo wa kutumia wasomi wa vyuo vikuu katika shule za msingi, kutokana na idadi
kubwa ya wahitimu wa ualimu, kutarajiwa kuwa kwenye soko la ajira.
Alisisitiza kuwa baada ya mwaka,
wahitimu wa vyuo vikuu watafundisha katika shule hizo na kwamba kufanya hivyo
si kuwashushia hadhi.
Akihutubia wananchi mjini Mbinga, kabla
ya kufungua kituo cha mabasi na barabara ya Peramiho- Mbinga yenye urefu wa
kilometa 78, Kikwete alisema barani Ulaya, hata walimu wa shule za chekechekea
wana Shahada na kwamba hicho ni kipimo cha maendeleo.
Kwa utaratibu uliozoeleka chini ya Sera
ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, walimu wa shule za msingi ni wenye
cheti.
Hata hivyo, kulingana na taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wapo wanaochukua Shahada, wanaosomea kufundisha elimu ya msingi.
Hata hivyo, kulingana na taarifa za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, wapo wanaochukua Shahada, wanaosomea kufundisha elimu ya msingi.
“Wakati umebadilika…leo utamchukua
Standard Seven ( Darasa za Saba) kwenda chuo cha ualimu? Leo Division Four
(waliopata Daraja la Nne) wanakataliwa vyuo vya ualimu,” alisema.
Alisema, hali ya sasa ni tofauti na
miaka ya nyuma kwa kuwa sasa, hata makatibu tarafa wana Shahada. Kwa mujibu wa
tamko la Serikali, kuanzia sasa wanaosomea ualimu ngazi ya Cheti na Stashahada,
sharti wawe na ufaulu wa daraja la tatu.
Aidha, Serikali imeamua kuanzia sasa
wanaojiunga na mafunzo ya Stashahada ya Ualimu katika masomo ya Sayansi wakiwa
na ufaulu wa Daraja la Kwanza, watasomeshwa bure. Pia wenye ufaulu wa Daraja la
Pili na la Tatu, watapewa mkopo.
Akizungumzia shule za sekondari za
kata, Rais Kikwete alipongeza maendeleo ya taaluma, kutokana na baadhi shule
hizo kuwa miongoni mwa wanaofanya vizuri katika mitihani ya taifa.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati
shule hizo zinaanzishwa, hali ilikuwa ngumu tofauti na sasa ambako yapo
mabadliko. Alitoa takwimu kwamba kati ya wahitimu 71,000 waliochaguliwa
kuendelea na Kidato cha Tano, 20,000 wameachwa.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na
wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari, Rais Kikwete aliagiza ifikapo
mwaka 2016, kila mwanafunzi awe na kitabu chake.
Alisema, serikali imeanza kutenga fedha
kwa ajili hiyo, zikiwemo Sh bilioni 21 zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu
wa fedha 2014/2015. Rais aliagiza fedha kwa ajili ya vitabu zitengwe na azione
kwa kuwa anataka taifa lipate wataalamu wengi.
Katika mkutano huo, Naibu Waziri wa
Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema katika shule za msingi hivi
sasa, wanafunzi watatu wanatumia kitabu kimoja.
Kwa mujibu wa Mhagama, kupitia Mpango
wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN), Wilaya ya Mbinga ilikuwa ya kwanza kitaifa kwa
maendeleo ya elimu.
Aliwapongeza walimu kwa kazi nzuri,
wanayofanya wilayani humo. Alibainisha kuwa walimu 112 waliopangiwa kufundisha
katika shule za msingi walikwenda, na wengine 138 waliotakiwa kwenda kufundisha
shule za sekondari, wanaendelea na kazi.
Credit: Habari leo
Credit: Habari leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAALIMU WENYE DIGRII MBIONI KUFUNDISHA SHULE ZA MSINGI.”
Post a Comment