Monday, July 28, 2014
WAZIRI MKUU AONYA MATUMIZI YA RUSHWA UCHAGUZI MKUU.
Do you like this story?
WAZIRI MKUU
Mizengo Pinda amewaonya Watanzania kuwa makini na watu wanaotumia rushwa ili
kupata nafasi za uongozi na hasa kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika
Oktoba, 2015.
Ametoa onyo hilo Julai 27, 2014) wakati akizungumza na mamia ya waumini na
viongozi mbalimbali waliohudhuria ibada ya uzinduzi wa dayosisi mpya ya Ruvuma
ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) na kuwekwa wakfu Askofu Amon
Mwenda aliyeteuliwa kuongoza dayosisi hiyo.
“Ninawasihi
wananchi wawe makini na viongozi wanaopenda kutoa rushwa hasa katika kipindi
hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu. Kama mtu ana nia ya kweli ya kuongoza
ni kwa nini atumie fedha ili kupata nafasi ya uongozi?,” alihoji.
“Tatizo ni
kwamba hata wananchi hivi sasa wanakubali kupokea kile kinachotolewa na
wagombea. Atakuja huyu atakupa hiki na mwingine naye atakupa kile, lakini ujue
akiingia madarakani anaanza kurudisha haraka vile alivyowagawia,” alisema.
Aliwaonya
wananchi kuwa makini ili wasije wakageuzwa mtaji wa kuwanufaisha watu binafsi.
“Tukikubali kutumika ni sawa tutapata viongozi wakati wa uchaguzi, lakini
watakuwa ni wale wasio na hofu ya Mungu, wenye kujali maslahi yao kuliko ya
wananchi waliowachagua,” aliongeza.
Aliwaomba
viongozi wote wa dini waliohudhuria sherehe hizo pamoja na waumini wote
waendelee kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na janga hilo la watu kupenda
rushwa. Alitumia fursa hiyo pia kuwaomba wazidi kuuombea mchakato wa kupata
Katiba mpya ili wabunge wote warejee ndani ya Bunge na kuikamilisha kazi
waliyoianza.
Alimuomba
Askofu huyo mpya apokee jukumu hilo kwa mikono miwili na kumuahidi kuwa kama
Serikali watakuwa naye bega kwa bega kuwaongoza Watanzania walioko kwenye
dayosisi yake. Dayosisi hiyo mpya inahusisha mkoa wote wa Ruvuma na wilaya ya
Ludewa eneo ambalo lina ukubwa wa kilometa za mraba 72,630. Kati ya hizo km. za
mraba 64,233 ni za mkoa wa Ruvuma na km. za mraba 8,397 ni za wilaya ya Ludewa.
Mapema,
akitoa hotuba yake ya kwanza mara baada ya kusimikwa rasmi, Askofu Mwenda
alisema dayosisi mpya ya Ruvuma imezaliwa katika kipindi chenye changamoto
nyingi za kidunia na utandawazi ukiwemo mmomonyoko mkubwa wa maadili.
Hata hivyo,
akiainisha malengo ya dayosisi hiyo ambayo anakuwa Askofu wake wa kwanza,
Askofu Mwenda alisema mbali ya kufundisha neno la Mungu, dayosisi hiyo
itahimiza ufanyaji kazi ili wakazi wake wawe na akiba ya chakula cha kutosha.
Alisema
watashirikiana na Serikali na wadau wa ndani najje katika kutoa huduma za
kijamii hasa elimu na afya. Aidha alisema atakabiliana na changamoto za sasa
ambazo alizitaja kuwa ni mmomonyoko wa maadili, rushwa, mauaji ya albino,
unajisi wa watoto na ubakaji wa wanawake.
Akitoa
shukrani kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Askofu Mkuu wa KKKT, Dk. Alex
Malasusa alisema Kanisa lingependa kupata viongozi ambao ni wacha Mungu.
Akirejea mahubiri yake, Askofu Malasusa alisema inashangaza kuona kuna baadhi
ya watu wanagombea nafasi za uongozi lakini hawana mapenzi na Mungu aliyewaumba
watu anaotaka kuwaongoza.
“Bila kujali
imani ya mtu, tunatamani tungepata kiongozi ambaye anamcha Mungu. Awe anapenda
kuhudhuria ibada. Awe anampenda Mungu ndipo atawapenda watu anaowaongoza,”
alisisitiza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WAZIRI MKUU AONYA MATUMIZI YA RUSHWA UCHAGUZI MKUU.”
Post a Comment