Thursday, July 17, 2014

WAZIRI MKUU PINDA KUWA MGENI RASMI KUMBUKUMBU YA CHIFU MKWAWA MKOANI IRINGA.



WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda anatarajia kuwaongoza wanakijiji cha Kalenga na Mkoa wa Iringa katika kilele cha maadhimisho ya kumbukumbu ya aliyekuwa Chifu wa Wahehe, Mkwawa itakayofanyika kijijini hapo Julai 19.

Siku moja kabla ya kilele hicho kutakuwa na kongamano la wazi litakalofanyika katika Chuo Kikuu cha Mkwawa likijadili namna ya kutangaza utalii wa Iringa na kumuenzi chifu huyo aliyepambana kuwaondoa Wajerumani.

Kwa mujibu wa waratibu wa siku hiyo, ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa maadhimisho hayo yatafanyika kila mwaka kuanzia mwaka huu licha ya kutofanyika mwaka jana kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi hayo, John Kiteve alisema mwaka huu yanafanyika baada ya wadau mbalimbali kuchangia.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCO), Gibson Sanga ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo alisema chuo chao kupitia mradi wake wa Kuendeleza Utamaduni Nyanda za Juu Kusini kimechangia sh milioni 16 ili kufanikisha kumbukumbu hiyo muhimu.

Jina halisi la shujaa huyo aliyejinyonga akiepuka kuuawa na Wajerumani ni Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga Mkwawa alizaliwa mwaka 1855 na kufariki Julai 19, 1898.

Historia ya shujaa huyo wa Wahehe itaendelea kubaki kutokana na umahiri wake wa kutaka kuwaondoa wakoloni katika ardhi ya Tanganyika mwishoni mwa karne ya 19.

NA DENIS MLOWE

0 Responses to “WAZIRI MKUU PINDA KUWA MGENI RASMI KUMBUKUMBU YA CHIFU MKWAWA MKOANI IRINGA.”

Post a Comment

More to Read