Friday, August 1, 2014
WATENGENEZAJI WA FILAMU HIZI WACHUKULIWA HATUA NA BODI YA FILAMU TANZANIA.
Do you like this story?
Na Benedict Liwenga.
Bodi ya Filamu, katika
ukaguzi wake wa kawaida uliofanyika tarehe 13 na 14 mwezi Machi, 2014, dhidi ya
filamu zinazoingizwa sokoni bila kufuta utaratibu, imeweza kukamata filamu
ambazo zilikuwa zimeingizwa sokoni bila kufuata taratibu, ikiwemo kukaguliwa na
Bodi ya Filamu, kuwekewa madaraja na kupewa vibali.
Filamu zilizogundulika
zikiwa sokoni ni Baunsa Kinyambe, Kanga Moko, Laki si Pesa, Muuza Genge na Mche
wa Sabuni ambapo Bodi ilichukua hatua ya kuwatafuta wahusika, na kupitia
matangazo ya filamu hizo walielekezwa kuziwasilisha kwa ukaguzi pamoja na
kuacha kuendelea kuzisambaza hadi zitakapokaguliwa na kupewa vibali.
Kukamatwa kwa filamu hizo
kunatokana na ukaidi wa wahusika kutowasilisha kazi zao kama walivyoelekezwa
hapo awali licha ya kutumiwa ujumbe kwa njia ya simu.
“Tarehe 15/04/2014,
wahusika tuliwatumia ujumbe kwa njia ya simu ili kuwakumbushia kuziwasilisha
kazi zao lakini hawakujibu ujumbe huo na baada ya jitihada mbali mbali za
kuwatafuta, wahusika hawa waliziwasilisha tarehe 31/07/2014”. Alisema Bi.
Fissoo
Akizungumzia waliowasilisha
kazi zao katika Bodi ya Filamu ni Jemedari Entertainment, ikiwakilishwa
na Mpole Gwatwambililege ambaye ndiye mmiliki wa Kampuni hiyo pamoja na Bwana
Geofrey Shaaban aliyeiwakilisha Tanzania Commedian Unit.
Wahusika hawa walitoa
ufafanuzi ufuatao kwa Bodi ya Filamu kuhusu uwepo wa filamu hizo na
kutokukaguliwa kwake huku zikiwa zimeshasambazwa na kwa upande wake Mmiliki wa
Jemedari Entertainment, Bwana Mpole Gwatwambililege aliieleza Bodi kuwa
mwanzoni mwa mwezi Machi 2014 alipigiwa simu na Bodi ya Filamu ikimtaka
awasilishe filamu tajwa kwa ukaguzi huku akisema kuwa kwa wakati huo
alipopigiwa simu alikuwa safarini nje ya Dar es Salaam na alirudi Dar es Salaam
mwezi Julai 2014 na alipofika Dar es Salaam aliwasili Bodi ya Filamu na
kuelekezwa kuwasilisha filamu husika kama alivyotakiwa na Bodi.
“Ilinilazimu kwenda sokoni
kuzitafuta filamu hizo na kufanikiwa kuzipata ingawa kwa maelezo niliyoyapata
kutoka sokoni nilielezwa kuwa msambazaji wa filamu hizo tano ni wale wale
wasambazaji niliowapa kazi ya kunisambazia filamu ya Mr. Damian ambayo
niliitengeneza awali iliyopewa kibali Na. 0003450 na Wasambazaji hao ni
Tanzania Comedian Unit”.Alisema Gwatwambililege.
Bwana Gwatwambililege
aliongeza kuwa ilimlazimu kuwatafuta vijana waliozisambaza filamu hizo tano na
kuwahoji ambapo wao walimueleza kuwa aliyewaelekeza kusambaza filamu hizo ni
Bwana Duncan Simon na kwa maelekezo ya Bwana Duncan Simon, wakatengeneza filamu
tano ambazo ni Baunsa Kinyambe, Kanga Moko, Laki si Pesa, Muuza Genge na
Mche wa Sabuni.
Kwa mujibu wa taarifa ya
Kikao kilichofanyika kati ya Bodi ya Filamu na wahusika taarifa inaeleza
kwamba, kabla ya safari, Bwana Mpole Gwatwambililege aliwapa Tanzania Commedian
Unit kazi ya kuisambaza filamu ya Baunsa Kinyambe huku akiwa amewaelekeza
kuiwasilisha Bodi ya Filamu kwa Ukaguzi kwanza. Wahusika aliowapa kazi ya
kuisambaza hawakuiwasilisha Bodi kwa Ukaguzi na wala hawakuisambaza filamu hiyo
kwa taratibu walizoelekezwa bali walinakili baadhi ya vipande vyake na
kuichanganya na Filamu za Muuza Genge na Mche wa Sabuni. Baada ya
hapo walitengeneza filamu nyingine mbili, yaani Kanga Moko na Laki si Pesa na
kuziingiza zote sokoni.
Kwa upande wao Tanzania
Commedian Unit ambayo iliwakilishwa na Geofrey Shaaban walikili wakisema kuwa
maelezo yaliyotolewa na Jemedari Entertainment yapo sahihi na hawahitaji
kuongeza au kukana kitu chochote.
Katika kikao hiko Bi.
Fissoo alifafanua kuwa, Tasnia ya Filamu inasimamiwa na Sheria ya Filamu na
Michezo ya Kuigiza Na. 4 ya 1976 na Kanuni zake Na. 156 za mwaka 2011. Hivyo,
wahusika wanatakiwa kufahamu kuwa kuingiza filamu sokoni bila kufuata taratibu
ni kosa kwa mujibu wa Sheria tajwa na Kanuni zake.
“Kikao kimepitishwa katika
vifungu mbali mbali vya Sheria na Kanuni zinazoelekeza hatua zinazopaswa
kufuatwa na hatua zinazochukuliwa dhidi ya wale wasiofuata taratibu, vifungu
hivi vya Sheria ni Kifungu cha 3 hadi cha 6 kikisomwa pamoja na kifungu cha 4
cha Kanuni za Sheria hiyo, vifungu vya 14 hadi 18 vya Sheria kuhusu ukaguzi wa
filamu vikisomwa pamoja na kifungu vya 25 mpaka 27 na kifungu cha 47 (1 na 2 A
mpaka C vya Kanuni za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza. Aidha,
Tanzania Comedian Unit, walijulishwa bayana kuhusu kughushi alama ya ukaguzi ya
kazi nyingine na kuiweka katika kazi tofauti suala ambalo litapeleka kwenye
kikao cha Bodi kitakachofuata”.Alisisitiza Bi. Fissoo.
Filamu za Kanga Moko na
Laki si Pesa zilishapigwa marufuku. Kuendelea kuwepo sokoni ni kukiuka
Sheria, Kanuni na Taratibu na pia utengenezaji na uingizaji filamu sokoni bila
kufuata taratibu ni kosa na kwa mujibu wa kifungu cha 47 (a 1 na 2 na b. 1) cha
Kanuni za Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza ya 1976, ambapo vimeipa Bodi
Mamlaka ya kuamuru kusitisha filamu hizo. Hivyo, Kifungu cha 32 kimeipa Bodi ya
Filamu mamlaka ya kuikubali au kuikataa filamu yoyote baada ya kuikagua. Kwa
mujibu wa kifungu cha 47, 1 na 2 wahusika wametakiwa kulipa faini ya papo kwa
papo ya shilingi milioni moja kwa kila kampuni kama ilivyofafanuliwa
katika vifungu vya Sheria.
Aidha, Filamu za Baunsa
Kinyambe, Muuza Genge na Mche wa Sabuni zitapitiwa na kutolewa maamuzi na Bodi
ya Filamu hivyo haziruhusiwi kwenda sokoni mpaka zitakapokaguliwa na kupewa
kibali. Bodi imewataka wahusika pia watafute muda wao kwa kutumia vyombo vya
habari wawaombe radhi watanzania kwa kuwapelekea kazi tukanishi na Nakala hiyo
ya kuomba radhi iwasilishwe Bodi ya Filamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ WATENGENEZAJI WA FILAMU HIZI WACHUKULIWA HATUA NA BODI YA FILAMU TANZANIA.”
Post a Comment