Friday, August 1, 2014

WAZIRI MKUU PINDA ATOA SAA 30 KUPEWA MAJIBU KWANINI MAELEKEZO ALIYOTOA KUHUSU KIWANDA CHA NYAMA MBEYA HAYAJAFANYIWA KAZI.



Mkuu wa mkoa Mbeya Abbas Kandoro akisoma taarifa fupi ya uwekezaji wa mkoa wa Mbeya




WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ametoa saa 30 na kutaka kupatiwa majibu ni kwa nini maelekezo aliyotoa kuhusu kiwanda cha kusindika nyama cha Mbeya hayajafanyiwa kazi.

Ametoa kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Agosti Mosi, 2014) wakati akizindua Kongamano la siku tatu la Uwekezaji la Mikoa ya Iringa, Njombe na Mbeya la mwaka 2014 ambalo limeanza leo kwenye ukumbi wa Benjamini Mkapa jijini Mbeya.

“Mbeya inaweza kuwa na fursa kubwa ya viwanda vya usindikaji nyama, unga wa mahindi ili kuongeza thamani ya mazao mnayozalisha katika mkoa wenu. Nilipokuwa hapa ziara yangu ya mwisho 2012, niliagiza kiwanda hiki kitafutiwe mwekezaji ili kianze uzalishaji. Jana nimeuliza kiwanda cha nyama kimefikia wapi, naambiwa watu bado wanaongea. Wanaongea nini?,” alihoji.

“Mtu akija kusikia habari ya kiwanda hiki atatuona ni wajinga tena ni wajinga wa kujitakia, kisa watu bado wanazungumza… hiki kiwanda cha nyama ni cha Mbeya na manuafaa yake ni kwa ajili ya wana Mbeya. Hivi wahusika ni kwani hamuioni hiyo fursa?” alisema.

“Dk. Mary Nagu watafute watu wa CHC waje hapa kujieleza ni kwa nini suala hili limechukua muda mrefu. Kabla sijaondoka hapa Mbeya kesho nataka nipate majibu kuhusu jambo hili,” aliagiza.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri Mkuu alisisitiza suala la watendaji wa mikoa na wilaya kuchukulia kwa umakini suala la uwekezaji kwani wasipofanya hivyo wao ndiyo watageuka kikwazo na kukwamisha maendeleo ya wananchi wanaowaongoza.

“Ndugu zangu wa Serikali za mitaa msiwe vikwazo, kuwezi wawezeshaji. Ninyi si watawala bali ni waleta maendeleo kwa jamii. Natoa wito mshirikiane na wafanyabiashara kuharakisha maendeleo ya wananchi mliokabidhiwa kuwaongoza. Acheni kudai hongo, kwani badala ya kuwasadia jamii, mtajikuta ninyi ndo mnakuwa vikwazo vya maendeleo,” alionya.

Alisema Serikali za Mitaa zinapaswa kuwa wawezeshaji na siyo wakwamishaji wa masuala ya maendeleo na ili kufanikisha hilo aliwataka wakuu wa mikoa waanzishe one-stop centre katika ngazi ya mkoa na Halmashauri ili wawekezaji wanapofika katika mikoa yao wasizungushwe na kukatishwa tamaa kwa sababu ya mlolongo wa taasisi zilizopo.

“Uzoefu unaonyesha kuwa baada ya kufanya makongamano kama haya, wawekezaji wengi wanajitokeza lakini katika ngazi ya Mkoa na Halmashauri wanakosa mahali ambapo wanaweza kushughulikiwa na kupata huduma bora kwa pamoja “One Stop Centre”. Hali hiyo huwafanya wakate tamaa.”
“Ninashauri kila Mkoa na kila Halmashauri iweke mfumo mzuri wa kuwapokea wawekezaji hususan kuwa na Mratibu (Focal Point) wa masuala ya uwekezaji ambaye ndiye atakuwa “One Stop Centre” wa kushughulikia wawekezaji wanaojitokeza na kuwahudumia kwa ufanisi bila urasimu. Ni imani yangu kuwa tukifanya hivyo, tutawezesha Kanda hii kuwa kitovu kikubwa cha uwekezaji katika nchi yetu,” aliongeza.

Alisema kila mmoja hana budi kuendelea amani na utulivu wa nchi ili uwekezaji uweze kufanikiwa na kushamiri. “Hakuna uwekezaji endelevu na wenye tija katikati ya fujo na migogoro, na uwekezaji utashamiri pale tu penye amani na utulivu,” alisisitiza.
Mapema, Waziri wa Nchi (OWM-Uwezeshaji na Uwekezaji), Dk. Mary Nagu alisema ili uwekezaji uweze kuwanufaisha wananchi, ni lazima rasilmali za nchi zigeuzwe kuwa bidhaa. “Ukiangalia chuma cha Liganga kipo pale miaka mingi, bila kukigeuza kuwa bidhaa, bado hakiwezi kuwanufaisha wananchi wetu,” alisema. Alisema bila uwekezaji hakuna uchumi, na bila uchumi hakuna maendeleo na bila maendeleo hakuna maisha bora kwa kila Mtanzania.

Katika hatua nyingine, Wakuu wa mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe walipewa nafasi ya kuzungumza na washiriki wa kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuelezea fursa mahsusi zilizomo kwenye mikoa yao.

Mada zitakazowasilisha katika kongamano hilo ambalo kaulimbiu yake ni“Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii katika Nyanda za Juu Kusini” zinahusu fursa za uwekezaji katika sekta za uchumi na miundombinu katika kanda hiyo, fursa za uwekezaji katika sekta za huduma za jamii katika kanda hiyo, fursa za uwekezaji katika kilimo cha mazao ya bustani (matunda, mboga, maua na viungo) na mchango wa taasisi za fedha katika uwekezaji.

Nyingine ni mchango wa sekta binafsi katika uwekezaji, na nafasi ya MKURABITA katika kukuza mitaji ya uwekezaji.

0 Responses to “WAZIRI MKUU PINDA ATOA SAA 30 KUPEWA MAJIBU KWANINI MAELEKEZO ALIYOTOA KUHUSU KIWANDA CHA NYAMA MBEYA HAYAJAFANYIWA KAZI.”

Post a Comment

More to Read