Thursday, August 7, 2014
RAIS BUSH AMSIFIA MAMA SALIMA KIKWETEKUTOKANA NA JITIHADA ANAZOZIFANYA ZA KUHAMASISHA WANAWAKE KUPIMA UGONJWA WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI
Do you like this story?
Na Anna Nkinda – Maelezo,
Washington
Rais wa zamani wa Marekani George
W. Bush amempongeza Mke wa Rais Mama Kikwete kutokana na kazi nzuri anayoifanya
ya kuhamasisha jamii na wanawake kwa ujumla kujitokeza kwa ajili ya kupima
saratani ya matiti na mlango wa kizazi.
Pongezi hizo zilitolewa jana na
Rais huyo mstaafu ambaye pia ni mwanzilishi wa Taasisi ya George W. Bush wakati
akifungua mkutano wa wake wa Marais wa Afrika uliofanyika katika ukumbi
wa mikutano uliopo kituo cha Kennedy (Kennedy Center) kilichopo
mjini Washington.
Mzee Bush alisema Taasisi yake
inasimamia mradi wa upimaji wa saratani ya matiti na mlango wa kizazi, ili nchi
za Afrika ziweze kupunguza idadi ya wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa
huo na hadi sasa zaidi ya wanawake 100000 wamefanyiwa uchunguzi katika nchi za
Tanzania, Zambia na Botswana lakini tatizo lililopo ni unyanyapaa kwa
wagonjwa wanaukutwa na tatizo hilo.
Alisema uchunguzi huo umefanyika
kwa kipindi cha miaka mitatu kwani saratani ya mlango wa kizazi ni moja kati ya
magonjwa makubwa yanayoua wanawake wengi katika nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa
la Sahara kwakuwa wanawake wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) wako
katika hatari kubwa zaidi ya kuugua ugonjwa huo.
Taasisi ya George W. Bush
inafadhili mradi wa Utepe wa Pinki Utepe Mwekundu (PRRR) ambao ndiyo wasimamizi
wa mradi huo uliogharibu zaidi ya dola za kimarekani milioni mbili ambao
pia utazinduliwa hivi karibuni katika nchi za Namibia na Ethiopia na zikufanya
nchi zinazofadhiliwa kufikia tano.
“Tatizo kubwa ni Ujinga ,
upatikanaji wa taarifa zisizo sahihi na unyanyapaa vinazuia maendeleo
ya afya ya jamii na hivyo wanawake kushindwa kwenda kupata chanjo ya
kuzuia ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi (Human Papilloma Virus Vaccine)
lakini watu wengi wanakufa kutokana na unyanyapaa ambao uko juu. Naamini
unaweza kuvunjwa mara moja kama kioo”, alisema Mzee Bush.
Aliwahimiza wake hao wa Marais
kuungana kwa pamoja ili kuweza kuimarisha afya ya mama na wasichana kwani
njia moja ya kuwasaidia watoto ni kuwasaidia mama zao. Na kusisistiza
kwamba ni jambo la muhimu kwa watu wanaoishi na VVU kutokufa kwa magonjwa
yanayoweza kutibika na kuzuilika.
Kwa upande wake Mke wa Rais wa
Marekani Mama Michelle Obama alisema wake wa Marais wa Afrika wana kazi kubwa
ya kuzisaidia jamii zao kutokana na matatizo yanayowakabili kwani
wanawake wengi na watoto wanakabiliwa na changamoto mbalimbali hasa za afya na
elimu.
Kwa upande wa vijana
alisema wanafanya kazi sana katika jamii lakini bado wanakabiliwa na changamoto
nyingi zikiwemo za ugonjwa wa Ukimwi. Wao kama viongozi wanatakiwa
kuhakikisha kuwa matatizo yao yanatatuliwa.
“Tunaweza kuwakusanya watu hawa
katika meza moja ili kuweza kutatua changamoto zao, nyie ni sauti za
wanyonge wakiwemo wanawake na watoto jitahidini kuwafikia wanawake wengi zaidi.
Wakati tunatoa kipaumbele kwa
wasichana wetu tunakazi kubwa ya kufanya naamini majadiliano haya yatatoa
jitihada mpya na nini cha kufanya ili tuweze kuwasaidia vijana wetu, ” alisema
Mama Obama.
Mama Salma Kikwete ni mmoja wa
wake wa Marais wa Afrika waliohudhuria mkutano huo uliandaliwa na Mke wa Rais
wa Marekani Mama Michelle Obama kwa kushirikiana na Taasisi ya George W.
Bush ambao ulijadili uwekezaji katika elimu, upatikanaji wa afya ya
wanawake na wasichana na kuimarisha mahusiano kati ya sekta za umma na binafsi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “RAIS BUSH AMSIFIA MAMA SALIMA KIKWETEKUTOKANA NA JITIHADA ANAZOZIFANYA ZA KUHAMASISHA WANAWAKE KUPIMA UGONJWA WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI”
Post a Comment