Wednesday, August 13, 2014
WANANCHI WAFANYA MAANDAMANO NA KUUA MBWA WALIOMUUA MWANAFUNZI NA KUMLA NYAMA.
Do you like this story?
Mbwa waliomuua mwanafunzi Ibrahimu Chipungahelo wakiwa wameuwawa na wananchi wenye hasira kali. |
Mmoja wa Mbwa wanaodaiwa kumuua marehemu Iblahim Faraja Chipungahelo ameuwawa. |
Hapa wananchi wakiwachoma moto mbwa hao |
Waitaka serikali kumuondoa OCD kwa kushindwa kulinda raia na mali zao
.DC aagiza hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika
Na Bazil Makungu Ludewa na
Nickson Mahundi.
Wananchi wa kata ya Ludewa
wameungana pamoja kufanya maandamano ya kushinikiza mbwa waliomuua mtoto na
kumtafuna wanauawa baada ya mmiliki wa mbwa hao kutishia kuwashtaki watakao
husika kuwaua mbwa wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti
katika mkutano wa dharula ulioitishwa na Diwani wa kata ya Ludewa Mama Monica
Mchilo walisema Mbwa hao wamekuwa tishio kwa muda mrefu kwani wameshateketeza
mifugo mingi wakiwemo mbuzi lakini cha kushangaza kila wanapolipeleka suala
hilo katika vyombo vya dola mmiliki huwaeleza walete ushahidi.
Kutokana na hali hiyo tata mkuu wa wilaya ya Ludewa Juma Madaha ameviagiza vyombo husika ikiwemo idara ya kilimo na mifugo, jeshi la polisi kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote anayehusika na tukio hili akiwemo mmiliki wa mbwa hao Bosco Thobias Lingalangala kwa sababu hakuna mtu aliye juu ya sheria.
Juhudi za kumpata mmiliki wa mbwa hao Lingalangala(BOLI) ambaye aliwahikuwa kiongozi wa klabu ya yanga miaka ya nyuma hazikuzaa matunda kutokana na simu yake kutopokelewa na baadaye kuzimwa kabisa.
Hali hiyo imejitokeza tena kwa
mmiliki wa mbwa hao alipoelezwa kuwa wamefanya mauaji na kumla mtoto wa darasa
la tatu katika shule ya msingi Ludewa mjini aliyefahamika kwa jina la Ibrahim
Chipungahelo(9)aliwataka wananchi kuleta ushahidi licha ya kuwa Askari wa jeshi
la polisi kwa kutumia silaha na kuuokoa mwili wa mtoto huyo ukiwa tayali
umeshaliwa katika baadhi ya viungo.
Akiongea katika mkutano huo mwenyekiti
wa Serikali ya Kijiji cha Ludewa Bw.Omary Kiowi alisema tukio na kauli za
mmiliki wa Mbwa hao wawili Bw.Bosco Lingalangala hazivumiliki kwa wanaludewa
kwani amekuwa akiwatishia wananchi kwa kutumia bastola kila wakati hivyo kikao
hicho kiliamuru mbwa hao wauawe na mmiliki achukuliwe hatua za kisheria.
“Tokea nizaliwe zijawahi kuona
Mbwa akitafuna mtu, hii ni mara ya kwanza,hatuwezi kuvumilia na ninachokiomba
wananchi msifanye fujo naamini tukitoka hapa kwa kushirikiana na ofisi ya
mifugo pamoja na jeshi la Polisi tunakwenda kumuua mbwa aliyebaki na tunamtaka
Bw.Bosco atushtaki wananchi wote na Serikali yetu kwa sababu anadhani yeye yuko
juu ya sheria”,alisema Bw.Kiowi.
Kufuatia kauli za vitisho
wananchi wakaomba kikao kiahirishwe na kuanza maandamano kuelekea katika nyamba
ya mmiliki wa mbwa hao ambako aliuawa marehemu Ibrahim na kuhakikisha wananmuua
mbwa aliyebaki kwa kupigwa risasi,kwa hasira walizo kuwa nazo wananchi hao
waliamua kuondoka na Mbwa hao wote wawili wakiwa wamekufa na kupita nao mitaani
huku wakiimba nyimbo mbalimbali.
Baada ya kuzunguka na mizoga ya
mbwa hao mitaani kwa muda mrefu hatimaye walielekea katika ofisi ya kata na
kuamua kuwachoma moto na kuwateketeza kabisa na kuendelea na kikao ambacho
kiliibua shangwe na vifijo baada ya mzee Laurance Mtweve (Muhuchu) ambaye ni
mzee mashuhuri kutoa kauli ya kuutaka uongozi wa kijiji kumuandikia barua mkuu
wa wilaya ya Ludewa ya kufukuza Bosco kuishi eneo la Ikilu kutokana na vitisho
vyake.
Mzee Muhuchu alisema kama uongozi wa wilaya utashindwa kufanya hivyo basi wazee wa wilaya ya Ludewa watamuandikia barua Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete kuwa wamechoshwa na unyanyasaji wa Bw.Bosco hiyo hawamuhitaji wilayani hapa tena.
Alisema kwani imekuwa kawaida
yake kuwatisha wananchi kwa kutumia bastola hali inayowafanya wananchi kuishi
kwa kuhofia usalama wao kwani inaonekana yuko juu ya sheria kutokana na kufanya
matukio ya ajabu lakini wanaoshtaki hupuuzwa na jeshi la polisi hapa Ludewa.
Aidha Diwani wa kata ya Ludewa
kupitia CCM mama Monica Mchilo aliwataka wananchi kupunguza jazba wakati sheria
inachukua mkondo wake ingawa awali alionesha kutoridhishwa na kauli za mmiliki
wa mbwa hao kuwa atawashtaki watakaohusika kuwaua.
Mama Mchilo alisema hakuna
aliyeridhishwa na kauli mbaya za Bosco lakini anaamini Serikali ni sikivu
itasikia kilio cha wananchi wa kata ya Ludewa kutokana na vitisho vya mtu huyo
ambaye hana hata chembe ya utu kwa kusema mbwa wasiuawe bali atawalipa fidia
wafiwa.
Aliwashukuru wananchi kwa kufanya
maandamano ya amani ambayo hayakuleta madhara kwa jamii lakini yalifanikisha
kuwaua mbwa ambao walikuwa ni tishio kwa jamii hasa kwa wanafunzi wanaopita
eneo hilo ambako aliwafugia mbwa hao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “WANANCHI WAFANYA MAANDAMANO NA KUUA MBWA WALIOMUUA MWANAFUNZI NA KUMLA NYAMA.”
Post a Comment