Tuesday, September 23, 2014
BUNGE LAPITISHA UPIGAJI KURA KWA FAX NA EMAIL
Do you like this story?
Bunge la Katiba
limeingia katika historia baada ya kupitisha kanuni zinazoruhusu wajumbe wake
watakaokuwa nje ya nchi kupiga kura kwa njia ya nukushi (fax) na baruapepe
(email).
Uamuzi huo ulifikiwa
bungeni Mjini Dodoma, baada ya wajumbe wa Bunge hilo kupitisha azimio la kuzifanyia
marekebisho kanuni ya 30, 36 na 38 za Bunge hilo za mwaka 2014.
Hata hivyo, wajumbe
watatu kati ya 15 waliochangia azimio hilo, walipinga vikali marekebisho hayo,
lakini yalipitishwa kwa wingi wa kura baada ya Mwenyekiti, Samuel Sitta
kulihoji Bunge.
Hii itakuwa ni mara
ya kwanza kwa raia wa Tanzania kupiga kura akiwa nje ya nchi, uamuzi ambao
Sitta aliutetea akisema wanaoupinga wanachanganya kati ya kura ya uamuzi na
kura ya uchaguzi.
Mwakilishi wa walimu,
Ezekiah Oluoch alisema Kifungu cha 16 (6) cha Kanuni za Bunge kinamtaka
mwenyekiti kuendesha Bunge kwa mujibu wa sheria walizonazo, Sheria ya
Mabadiliko ya Katiba na sheria nyingine za nchi.
“Hoja ya walioko nje
ya Bunge hili kupiga kura, siiungi mkono na wengi mkiunga mkono mtakuwa mmekiuka
sheria ... kila raia ana haki ya kupiga, Katiba yetu inaeleza, ilimradi atimize
miaka 18 lakini haki hiyo imewekewa pia utaratibu wa kisheria,” alisema.
Alisema kwa taratibu
zilizowekwa nchini, hakuna unaomruhusu mtu aliyeko nje ya eneo la kupiga kura
kufanya hivyo.
Hata hivyo, Sitta
aliingilia kati akisema mjumbe anasema uongo, akimtaka aeleze ni kura ipi
anayoizungumzia na kifungu gani kimesema hilo, naye akajibu kura anazozungumzia
ni zote ikiwamo ya kufanya uamuzi ndani ya Bunge.
“Unasema uongo mtupu
wewe ... sheria ya uchaguzi, tunamchagua nani hapa?” alihamaki Sitta na hali
kama hiyo aliionyesha pia kwa wajumbe wengine waliokuwa wakipinga marekebisho
hayo.
Oluoch alisema
anachoona ni kuwa si halali kwa mjumbe ambaye hayuko ndani ya Bunge kupiga kura
na kutaka Bunge lisifanye mambo kwa sababu linataka kutimiza mambo ambayo si
msingi wa sheria.
“Uamuzi wowote huo
tunaotaka kufanya kwa lengo la kupata utashi wa kisiasa, mimi nitasimama peke
yangu kukataa na itaingia kwenye hansard (kumbukumbu za Bunge) kwamba nilikataa
jambo hili,” alisema.
Kwa upande wake, Said
Arfi alisema hakubaliani na azimio hilo kwa sababu Kanuni ya 38 ilikuwa
imeshaweka utaratibu na haoni kuwapo haja ya kufanya marekebisho.
“Jambo hili
tunalofanya ni kubwa sana, kuandika Katiba ya Taifa letu ni lazima tuwe na nia
zilizokuwa njema ili kulipatia Taifa Katiba ambayo itaridhiwa na Watanzania.
Sioni sababu zozote za msingi kwa wajumbe ambao hawapo humu ndani kupiga kura.”
Arfi alisema uzoefu
wa mabunge mengi duniani wanaopiga kura ni watu waliomo ndani ya ukumbi wa
Bunge tu... “Sasa hii ya kwenda kuwatafuta watu huko waliko hauna uhakika
anayepiga kura ndiye, ni shaka tupu. Kwa kweli mheshimiwa mwenyekiti Watanzania
watatutazama juu ya nia zetu na dhamira zetu juu ya kulipatia Taifa Katiba
maridhawa,” alisema.
Alisema kura ni hiari
na mjumbe anaweza kuwapo ndani ya Ukumbi wa Bunge na kuacha kupiga kura na
kuonya kuwa kuwalazimisha na kuwatafuta watu ili wapige kura si jambo la
kidemokrasia.
Wakati akiendelea,
Sitta aliingilia kati na kumhoji nani anayelazimisha mtu kupiga kura? Arfi
akamjibu;
“Unapotuingilia
katika michango yetu Watanzania wanakupima. Watanzania wanakuheshimu
mwenyekiti.”
Kwa upande wake, Ali
Omary Juma alisema Katiba ni maridhiano ya nchi mbili huru na si busara
kuharakisha kupiga kura kwa watu ambao hawamo ndani ya Bunge.
Alisema kama hilo
litaruhusiwa itakuwa ni mgongano mkubwa wa kisheria ambao utaleta ufa mkubwa
kama uliojitokeza baina yao na Ukawa … “Nashauri suala la kura tulisitishe ili
kutoa fursa pana ya mashauriano na kutoa muda ili wajumbe wote tuhudhurie.”
Mjumbe Paul Makonda
aliunga mkono hoja hiyo akisema wajumbe zaidi 600 kuwa mahali pamoja si jambo
rahisi:
“Nakumbuka tukiwa
kwenye kamati yetu siku moja mtu alilazimika kutoka hospitalini. Ni mgonjwa
lakini afanyeje, lakini kama kuna uhuru wa kupiga kura pale alipolala ni jambo
la heri.
“Hatutafuti kura
mpya. Hapa tunatafuta kupiga kura kwa wale watu ambao walishajadili jambo hili,
haina maana tunatafuta kuokotaokota kama tumepungukiwa, hatujapungukiwa hata
kidogo.”
Baadaye Sitta
alisimama na kusema ipo dhana inayojengeka kwamba utaratibu huo unalenga
kulazimisha kila mjumbe kupiga kura ili tu theluthi mbili ipatikane, hivyo akataka
wajumbe waache kupoteza muda ... “Hii ni dhana ya ajabu na ina nia mbaya ndani
yake. Mmoja wa watu ambao ameomba apige kura yuko hospitali India, nina mamlaka
gani ya kumkatalia?”
“Tumempigia Balozi
atamwapisha atapiga kura ya siri italetwa na itafunguliwa humu. Zote hizo
zitafunguliwa humuhumu ndani ya ukumbi na majina yatasomwa,” alisema Sitta.
“Watakaopiga kura
mbele ya mabalozi wetu kwa wazi, Record (kumbukumbu) yote italetwa hapa na
mtashuhudia hapa majina yatatajwa moja moja kama kanuni zinavyotaka,” alisema
Sitta na kuongeza;
“Mambo haya ni ridhaa
ya mtu, hakuna mtu atalazimishwa. Kama kuna hao wanasimama hapa wanasema
wanalazimishwa, kama wameshindwa kuchangia hoja hii wasipoteze muda.”
Akijibu hoja za
wajumbe, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho alisema wakati wa
kuhakiki mjumbe halali, wale walioko watawasilisha pasi za kusafiria.
Wasomi wapinga
Akizungumzia uamuzi
huo, Profesa wa Chuo Kikuu cha Ruaha, Gaudence Mpangala alisema uamuzi huo ni
dalili za kupaparika kwa sababu kila kona Watanzania wanapinga kuendelea kwa
vikao vya Bunge hilo.
“Tanzania hatujafikia
hatua ya kuruhusu wananchi wapige kura wakiwa nje ya nchi yao, iweje leo
tukubali jambo hili kirahisi namna hii, kuna nini nyuma yake? Wanachokifanya bungeni
wananchi wanakifuatilia na watambue wazi kuwa hiyo Katiba watakayoipitisha
itapingwa.”
Mhadhiri Mwandamizi
wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema, “Kama wamekubaliana
kubadili kanuni sawa, ila lazima tujiulize kwa nini sasa. Kwa nini wabadili
kanuni hizi ili kupiga kura tu?”
Dk Bana alisema
hakuna ulazima wa kuharakisha mambo ili kupata Katiba Mpya kutokana na hali
halisi iliyopo sasa.
“Nasubiri kwa hamu
kuiona hiyo Rasimu wanayotaka kuipigia kura ili niilinganishe na iliyotolewa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Kuanzia hapo tutaanza kuhoji kama mambo yatakuwa
tofauti,” alisema.
Mwalimu wa Idara ya
Lugha za Kigeni na Isimu UDSM, Faraja Christoms alisema sheria za nchi
zinatakiwa kwenda sambamba na Katiba ambayo ni sheria mama, hivyo kuruhusu
upigaji wa kura wa aina hiyo ni kinyume na sheria.
Aliyekuwa rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Felix Kibodya alisema, “Unaweza
ukabadili kanuni lakini haitakuwa na maana kama hakutakuwa na maridhiano.”
Imeandikwa na Daniel
Mjema, Sharon Sauwa na Fidelis Butahe wa gazeti la Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)


0 Responses to “BUNGE LAPITISHA UPIGAJI KURA KWA FAX NA EMAIL ”
Post a Comment