Wednesday, September 24, 2014
MAJAMBAZI WAUA NA KUPORA KIBAHA MKOANI PWANI.
Do you like this story?
WATU wanne
wanaodhaniwa kuwa ni majambazi wanatuhumiwa kumwua mtu mwenye umri kati ya
miaka 35 na 40 ambaye jina lake halikuweza kufahamika na kumjeruhi mwingine.
Tukio hilo
lilifanyika kwenye maduka yaliyopo kwenye Stendi Kuu ya Maili Moja wilayani
Kibaha, jirani na kituo cha Polisi baada ya watu hao kufanya tukio la uhalifu.
Kutokana na tukio
hilo, Jeshi la Polisi mkoani Pwani lipo katika msako mkali wa watu hao
waliovamia duka liitwalo Bahati, mali ya Hashim Kisaka wakiwa na bunduki na pia
walivamia ofisi ya kukata tiketi ya mabasi yaendayo mikoani kisha kupora fedha
kwenye maduka hayo.
Akithibitisha kutokea
kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Athumani Mwambalaswa
alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 2 kasoro usiku Septemba 20
mwaka huu.
“Watu hao walivamia
katika maeneo hayo wakiwa na silaha ambayo bado haijafahamika na kumuua mtu
huyo kwa kumpiga na risasi ya kifuani kisha kumjeruhi mguuni mfanyabiashara wa
korosho Ambwene Mwambungu wakati wa tukio hilo ambalo lilifanyika huku umeme
ukiwa umekatika na hali iliyofanya kukawa na giza nene na watu hao kutumia
mwanya huo kutekeleza tukio hilo,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Alieleza kuwa, kwenye
tukio hilo watu hao wakiwa na silaha hiyo walivamia katika maduka hayo na
kuanza kupiga risasi hewani hali iliyowafanya watu waliokuwa katika eneo hilo
kukimbia hovyo huku wakiacha mali zao kuhofia usalama wao, kisha kupora fedha
na mali ambayo thamani yake bado haijafahamika.
“Marehemu alifikwa na
mauti wakati akipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi huku
majeruhi wa tukio hilo bado amelazwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha ya
mguu aliyoyapata,” alisema Kamanda Mwambalaswa.
Aliwataka wananchi
kushirikiana kwa pamoja kutoa taarifa mara moja watakapobaini walipo watu hao
pia kutoa taarifa mara wanapohisi watu wasioeleweka katika maeneo yao.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)

0 Responses to “MAJAMBAZI WAUA NA KUPORA KIBAHA MKOANI PWANI.”
Post a Comment