Tuesday, September 2, 2014
PINDUAPINDUA YA RASMU YA KATIBA
Do you like this story?
Dodoma. Bunge
Maalumu la Katiba linaanza vikao vyake tena leo mjini Dodoma, huku kukiwa na
jitihada kubwa za kujaribu kuweka udhibiti wa mjadala utakavyoendeshwa miongoni
mwa wabunge, wengi wao wakiwa ni kutoka chama tawala CCM.
Kuna hofu
ndani ya chama hicho kwamba mgawanyiko uliojitokeza wakati wa vikao vya kamati
utahamia kwenye Bunge zima ambako mbali na waandishi wa habari kuruhusiwa
kushiriki, pia huonyeshwa moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni.
Msigano
unaotabiriwa kutokea ni ule uliojengwa katika mambo yaliyozua mvutano ndani ya
kamati kiasi cha wajumbe wenye itikadi moja kusigana kwa misingi tofauti lakini
kubwa likiwa ni lile la Uzanzibari na Ubara.
Tofauti hizo
za kimaeneo zilionekana dhahiri wakati wa mjadala wa Sura ya Tisa na 10 ambazo
zinahusu muundo wa Bunge na mambo mengine ya utawala, pia katika Sura ya 14
hususan mgawanyo wa mapato.
Mwishoni mwa
wiki iliyopita, baadhi ya wenyeviti wa Kamati za Bunge hilo walitabiri mvutano
mkali bungeni, wakirejea hali ilivyokuwa ndani ya kamati zao ambako baadhi ya
wajumbe hawakuridhika na baadhi ya uamuzi.
Mwenyekiti wa
Kamati Namba Nne, Christopher Ole Sendeka alisema mjadala katika kamati yake
ulikuwa mkali na kwamba hali itakuwa ni ngumu zaidi watakapoingia bungeni.
Mwenyekiti wa
Kamati Namba Tatu, Dk Francis Michael alisema suala la ardhi linaweza kuzua
mvutano mkali kwani ni moja ya mambo muhimu katika Katiba.
Makamu
Mwenyekiti wa kamati Namba Kumi na Moja, Hamadi Yusufu Masauni alisema jambo
pekee analotarajia kuwa litasumbua ni muundo wa Bunge la Muungano.
Alisema
unapotajwa muundo wa Bunge ndipo unapotajwa mfumo wa Muungano ambao umekuwa ni
kero ya muda mrefu.
Mwenyekiti wa
Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu alisema hofu yake iko kwenye suala la mgawanyo
wa mapato ambalo kamati yake ilisita kulijadili hadi walipoitwa wataalamu
kutoka Benki Kuu ya Tanzania na Wizara ya Fedha za Muungano na ile ya Zanzibar.
Kwa msingi
huo, wakati kamati zikianza safari ya siku tano kuwasilisha taarifa zake
kuanzia leo hadi Septemba 8, mwaka huu, kutakuwa na maoni ya wachache katika
baadhi ya kamati suala ambalo linatoa picha ya kuwapo kwa mawazo tofauti katika
mambo kadhaa.
Uchunguzi wa
gazeti hili umebaini kuwa mengi ya mambo hayo ni yale yaliyobadilishwa kinyume
na yalivyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba iliyotungwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba au mambo mapya yaliyoingizwa kwenye rasimu hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “PINDUAPINDUA YA RASMU YA KATIBA”
Post a Comment