Wednesday, September 24, 2014
WANAFUNZI WA CHEKECHEA TUNDURU WASOMEA CHINI YA MTI.
Do you like this story?
![]() |
| Wanafunzi wa wa Chekechea wakiwa wamekaa chini |
WANAFUNZI
wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Nakayaya Wilaya ya Tunduru mkoani
Ruvuma wanasomea chini ya mti kutokana na darasa hilo kuendeshwa bila ya kuwa
na chumba maalum kwa ajili ya kusomea wanafunzi hao.
Hali
hiyo imebainika baada ya mwandishi wa habari hizi kuitembelea shule hiyo hivi
karibuni na kuwakuta wanafunzi wakiwa wamekaa chini huku wakiendelea na masomo
hayo nje chini ya mti ulio na kivuli cha kuwahifadhi wakati wa jua kali.
Akizungumza
shuleni hapo Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nakayaya, Christina Mhowera
alisema watoto hao wamelazimika kusomea nje baada ya huduma ya elimu hiyo
kuanzishwa shuleni hapo bila ya kuwa na jengo maalum kwa wanafunzi wa awali.
Alisema
awali wanafunzi hao walikuwa wakisomea kwenye gofu (jengo mbovu) lililokuwa
jirani na shule, lakini walilazimika kuondolewa baada ya jengo hilo kutwaliwa
kwa matumizi mengine. Aliongeza kuwa baada ya hapo walihamishiwa kwenye nyumba
ya mwalimu kabla ya kukamilika lakini waliondolewa tena na kuanza kusomea nje
(chini ya mti) hadi sasa.
Alisema
darasa hilo lenye jumla ya wanafunzi 92 linaendeshwa bila ya kuwa na chumba cha
darasa maalum wala madawati kutokana na shule hiyo kukabiliwa na uhaba wa
vyumba vya madarasa hadi hapo watakapopata darasa maalum kwa ajili ya wanafunzi
hao.
Aidha
uchunguzi uliofanywa katika shule nyingine tatu za Wilaya ya Tunduru, yaani
Shule ya Msingi Nanjoka, Majengo na Shule ya Msingi Tunduru Mchanganyiko
kuangalia mazingira ya utoaji elimu ya awali katika shule hizo umebainisha
kukabiliwa na changamoto nyingi hali ambayo inahatarisha msingi wa elimu kwa
wanafunzi.
Kwa
upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nanjoka, Batadhari Mkwela alisema
licha ya usajili wa wanafunzi wa awali kuongezeka kila mwaka kumekuwa hakuna
bajeti ya kuendesha elimu hiyo.
“…Darasa
la awali linahitaji vitendea kazi lakini havipo, hatuna vifaa kama vitabu vya
kutosha, vyenzo za kufundishia, hakuna bajeti hata ya vifaa hivi toka
Serikalini, hatuna madawati maalum kwa ajili ya wanafunzi wa awali,” alisema
Mkwela.
Akizungumzia
hali hiyo, Kaimu Ofisa Elimu Wilaya ya Tunduru, Abdul Kazembe alisema vyumba
vya madarasa ni changamoto kubwa eneo hilo licha ya msisitizo kuendelea
kutolewa wa kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali. Alisema mwaka 2013/14
halmashauri ya wilaya hiyo ilihitaji zaidi ya milioni 366.7 lakini ililetewa
zaidi ya milioni 196.5 fedha ambayo ni karibia nusu tu ya kiasi kilichopitishwa
kwenye bajeti hiyo.
“…Kwa
hiyo unaweza kuona kwamba ni ngumu kuigawa fedha hii katika matumizi maana
kwanza haitoshi na pili hata kilichotegemewa kuja ni pungufu zaidi tena sana,
sasa sijui unaweza kugawa kila shule ipate shilingi ngapi…kwani haitoshelezi,”
Abdul Kazembe.
Akifafanua
zaidi Kaimu Ofisa Elimu huyo alisema miundombinu ya madarasa ni changamoto
kubwa, kwani mwaka 2013 idadi ya mahitaji ya madarasa kwa wilaya nzima ilikuwa
ni 1,715 lakini madarasa yaliopo ni 900 na kitu huku mengine yakiwa ni ya muda
mrefu na yanaelekea kuchakaa.
*Imeandaliwa
na www.thehabari.com
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)



0 Responses to “WANAFUNZI WA CHEKECHEA TUNDURU WASOMEA CHINI YA MTI.”
Post a Comment