Wednesday, October 15, 2014

MKUU WA MKOA AKATAA KIINGEREZA KUTUMIKA KWENYE WARSHA, KISA WAJUMBE HAWAIELEWI HIYO LUGHA




MKUU wa Mkoa wa Singida, Dk Parseko Kone juzi alilmtaka mshereheshaji katika warsha ya wadau wa rasimu ya mpango wa usimamizi na uendelezaji wa pamoja wa rasilimali za maji Bonde la Kati kuacha kuendesha utambulisho wa wajumbe hao kwa lugha ya Kiingereza badala yake atumie Kiswahili.

Alilazimika kuingilia kati baada ya kushuhudia baadhi ya wajumbe waliokuwa wakitambulishwa na kutakiwa kusimama ili waonekane kushindwa kufanya hivyo kwa kile kilichodhihirika wazi kupigwa na bumbuwazi na utambulisho huo wa lugha ya Kiingereza.

Akionesha wazi kukerwa kwake na mshehereshaji, Dk Kone alisema wakati taifa liko katika juhudi za kukuza Kiswahili, baadhi ya Watanzania wanakwamisha juhudi hizo kwa sababu hafifu kama za kuwepo baadhi ya washiriki wasiojua Kiswahili.

“Wajumbe wa warsha hii wako 200 na wasioelewa Kiswahili ni wanne tu. Idadi hii ndogo haiwezi kusababisha mkutano huu uendeshwe kwa Kiingereza. Wengi wetu hapa japo tunajua Kiingereza, baadhi yetu mwaka umepita bila kukizungumza; hivyo inahitaji mtu kujiandaa ili kuwa katika nafasi nzuri ya kukizungumza,” alisema.

Aidha, alisema endapo warsha hiyo ingeendeshwa kwa lugha ya Kiingereza, wachangiaji wa rasimu hiyo wangekuwa wachache hivyo kuwanyima wengi fursa ya kutoa mawazo yao.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka wadau kushirikiana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili usimamizi wa rasilimali za maji kutokana na suala hilo kuwa mtambuka.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni migogoro inayohusu maji pamoja na siasa.

Alisema Sekta ya Maji ina jukumu kubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi, lakini kwa bahati mbaya inakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo bila kutatuliwa huathiri utekelezaji wa mipango na mikakati ya maendeleo na usimamizi wa rasilimali za maji.

Bonde la Kati lenye makao yake makuu mkoani Singida ni miongoni mwa mabonde tisa yaliyopo nchini na linajumuisha maeneo ya Dodoma, Manyara, Singida, Tabora, Shinyanga, Arusha na Kilimanjaro ambapo linagusa jumla ya wilaya 26. Ni la pili kwa ukubwa likiwa na kilomita za mraba 143,099.

0 Responses to “MKUU WA MKOA AKATAA KIINGEREZA KUTUMIKA KWENYE WARSHA, KISA WAJUMBE HAWAIELEWI HIYO LUGHA ”

Post a Comment

More to Read