Tuesday, October 7, 2014
POLISI WACHANA BANGO LA WALIMU LINALOHOJI POSHO ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA.
Do you like this story?
Maandamano ya walimu kuingia katika
Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kuadhimisha Siku ya Walimu Duniani, jana
yalipata mtafaruku baada ya polisi kuyaingilia na kuchana bango mojawapo
lililohoji posho za wajumbe wa Bunge la Katiba.
Bango hilo la kitambaa cheupe lilikuwa na maandishi yanayohoji posho ya
Sh300,000 waliyokuwa wanapata wajumbe wa Bunge la Katiba, yakilinganishwa na
kazi kubwa wanayofanya walimu.
Ujumbe wenyewe ulisomeka hivi:
“Haki iko wapi usawa uko wapi, posho ya mjumbe wa Bunge la Katiba kwa siku
shilingi laki tatu, mshahara wa mwalimu shilingi 370 kwa mwezi. No big results
without big salary (Hakuna matokeo makubwa bila mshahara mkubwa)”.
Ujumbe huo ulikuwa ukifanya rejea ya viwango vya malipo ya Sh300,000 kwa
siku ambazo walikuwa wakilipwa wajumbe wa Bunge Maalumu zikiwa ni Sh230,000
kama posho ya kujikimu na Sh70,000 ambazo ni posho ya vikao.
Hata hivyo bango hilo lilichanwa hatua chache kabla ya walimu hao
hawajaingia uwanjani humo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo
Pinda. Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), mkoani Kagera Dauda
Bilikesi, alisema amesikia habari za bango hilo kuharibiwa lakini akasema
asingezungumza kwa kina kuhusu suala hilo kwa kuwa hayo yamepita.
Waibuka na shairi
Muda mfupi baada ya polisi kuharibu bango hilo lisionekane uwanjani,
walimu hao walipiga chenga kiana wakaibuka na ujumbe ule ule kwa njia ya
shairi.
Kupitia shairi hilo liliposomwa mbele ya Pinda, walimu walihoji ukubwa wa
posho za wajumbe wa Bunge la Katiba zikilinganishwa na mshahara wanaopata, hali
iliyosababisha umati wa walimu uliokuwa uwanjani hapo kulipuka kwa sauti kubwa
za shangwe.
Shairi hilo lililosomwa na Mwalimu Betwel Magoso kutoka Wilaya ya
Biharamulo, lilisababisha kuvurugika kwa muda kwa utaratibu uliopangwa kwa
mujibu wa ratiba, pale alipohoji wajumbe wa Bunge la Katiba kupata Sh1 milioni kwa
siku tatu ambazo ni mkopo wa mwalimu kwa miaka mitatu.
Mwalimu Magoso alimgusa Pinda ambaye kabla ya kuanza hotuba yake alianza
kwa kusema kuwa mwalimu huyo alitumia ujanja kufikisha ujumbe wake na kuwa
baadhi ya maneno katika shairi lake yalikuwa ni mazito.
Kanuni za mafao zasitishwa
Katika hatua nyingine, Serikali imesitisha matumizi ya kanuni mpya za
ukokotoaji mafao ya pensheni ambao umeibua malalamiko kuwa malipo ya mkupuo
yalipunguzwa kutoka asilimia hamsini hadi ishirini na tano.
Kanuni hizo ni zile zilizotungwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii (SSRA) na kutangazwa Agosti 6, mwaka huu mjini Dodoma na
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
Tangu kutangazwa kwake kanuni hizo zilizua malalamiko kutoka kwa wadau
mbalimbali hususan wafanyakazi ambao walisema kuwa hayalengi kuboresha wala
kuhuisha mafao, bali yanapunguza stahili hiyo tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Akihutubia sherehe hizo, Pinda alisema suala hilo linarejeshwa tena
serikalini kuangaliwa upya.
“Acha suala hili tulirejeshe serikalini tukalitazame upya kwa sababu
halikubaliki na hatuwezi kulishurutisha kwa sababu nyie ndiyo wadau, siyo sisi.
Tutawaambia walitazame tena na warudi wawashirikishe vizuri wawaeleze mlikubali
au mlikatae,” alisema Pinda.
Waziri Mkuu alisema pamoja na kuwa lengo lilikuwa ni kuboresha maisha ya
wafanyakazi kwa kuleta mfumo mpya wa ukokotoaji wa mafao ya pensheni, suala
hilo lilihitaji ushirikishwaji mpana zaidi ikiwa ni pamoja na wadau wenyewe.
Katika kuunga mkono kilio cha walimu, Pinda alitoa mfano wa wabunge
wanaopata mafao yao yote wanapomaliza kipindi cha uwakilishi kwa miaka mitano
na kuwa kabla ya hapo mafao hayo yalitolewa baada ya kumaliza miaka kumi, jambo
ambalo halikupendelewa na wabunge.
Kauli hiyo ilitokana na risala ya walimu iliyosomwa na Katibu Mkuu wa
CWT, Yahya Msulwa aliyesema mabadiliko hayo yamezua manung’uniko makubwa hasa
kwa walimu wanaobeba idadi kubwa ya watumishi.
Alisema mfumo wa ukokotoaji wa mafao wa zamani, pamoja na kuwa mishahara
yao ni midogo, ulifanya mafao yao ya uzeeni yawe na unafuu kwa kiwango fulani,
ikilinganishwa na mfumo mpya ambao ukokotoaji unafanyika kwa kuangalia wastani
wa mishahara ya miaka mitatu ya mwisho.
Kabla ya mapendekezo hayo, ukokotoaji wa mafao ulifanyika kwa kuangalia
mshahara wa mwisho wa mtumishi na malipo yalitolewa kwa asilimia hamsini ya
mafao yote baada ya ukokotoaji kufanyika.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)


0 Responses to “ POLISI WACHANA BANGO LA WALIMU LINALOHOJI POSHO ZA BUNGE MAALUM LA KATIBA.”
Post a Comment