Monday, January 12, 2015

JK ATUMA UJUMBE MZITO DHIDI YA WATU WATAKAO VURUGA UCHAGUZI MKUU 2015




Rais Jakaya Kikwete ametuma ‘ujumbe mzito’ dhidi ya watakaofanya vurugu ama kuvuruga Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu, akisema watachukuliwa hatua kali.

Rais Kikwete, ambaye atakuwa akimaliza kipindi chake cha miaka kumi tangu akabidhiwe nchi mwaka 2005, ametoa kauli hiyo ikiwa ni wiki chache baada ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa kutawaliwa na vurugu na ukiukwaji wa sheria na taratibu na kusababisha wakurugenzi sita kutenguliwa ajira zao wakati wengine watano wakisimamishwa ili kupisha uchunguzi.

“Hatua za kinidhamu zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya watu waliovuruga Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwishoni mwa mwaka jana ni ujumbe mzito kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba,” alisema Rais Kikwete juzi wakati akizungumza na mabalozi wa nchi mbalimbali Ikulu jijini Dar es Salaam.

“Tunatuma ujumbe mzito kwamba matukio hayo hayatavumiliwa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015,” alisema Rais Kikwete.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Desemba 24, baadhi ya wafuasi wa vyama mbalimbali vya siasa, wamekamatwa na wengine kufikishwa mahakamani kutokana na kufanya vurugu wakati, kabla na baada ya uchaguzi huo.

Mbali na kukamatwa watu hao, Waziri wa Nchi Ofisi ya  Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Hawa Ghasia Desemba 17, 2014, aliwasimamisha kazi wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali kutokana na kuchelewa kuandaa na kupeleka vifaa vya kupigia kura.

Pia, walitimuliwa kazi kutokana na uzembe kutekeleza majukumu yao katika Uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba 14 na 20 mwaka jana.

Vyama vya siasa, CUFna Chadema vimeendelea kulalamikia matokea ya uchaguzi huo, ambao CCM ilipata ushindi mkubwa, lakini ikapoteza baadhi baadhi ya mitaa iliyokuwa ngome ya chama WRais Kikwete alisema licha ya vurugu katika baadhi ya maeneo nchini, Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umeonyesha kukua na kukomaa kwa demokrasia nchini.

Hata hivyo, tamko lake halikupokewa vizuri na viongozi wa vyama vya upinzani.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, John Mnyika, alisema badala ya kuzungumzia vurugu, Rais alipaswa kuwaeleza mabalozi amemchukulia hatua gani Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa kutengeneza kanuni mbovu zilizosababisha uchaguzi uvurugike.

“Aidha, alipaswa aeleze amemchukulia hatua gani Pinda kwa kujibu bungeni kuwa maandalizi yote ya uchaguzi yalikuwa tayari, ikiwamo bajeti kumbe hali ni tofauti na hivyo kuathiri upatikanaji wa vifaa na ubora wa uchaguzi,” alisema Mnyika.

Pia, alisema inawezekana wakurugenzi waliosimamishwa walikataa kutii maelekezo ya kuhujuhumu upinzani.

0 Responses to “JK ATUMA UJUMBE MZITO DHIDI YA WATU WATAKAO VURUGA UCHAGUZI MKUU 2015”

Post a Comment

More to Read