Thursday, January 22, 2015
SAKATA LA ESCROW : IKULU YAELEZAHATIMA YA KIPORO CHA MUHONGO, YASEMA RAIS KIKWETE ATATIMIZA AHADI HIVI KARIBUNI.
Do you like this story?
IKULU imewataka Watanzania kuwa na subira kwa kuwa Rais Jakaya Kikwete wakati wowote kuanzia sasa atatoa uamuzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Profesa Muhongo na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali
wanahusishwa na sakata la uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 kwenye akaunti
ya Tegeta Escrow.
Viongozi wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo,
Eliakim Maswi ambaye amesimamishwa kupisha uchunguzi, aliyekuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye amejiuzulu na aliyekuwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye tayari
uteuzi wake umetenguliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam
jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, alisema si kweli
Rais Kikwete anakwepa kumwajibisha Profesa Muhongo kama watu wengi wanavyodai.
Alisema kinachofanywa na Rais Kikwete ni kufuata utaratibu
unaotakiwa.
“Siku
mbili tatu alizosema rais maana yake ni hivi karibuni na msidhani anakimbia
kutoa uamuzi… siku si lazima zihesabike, ni siku yoyote atatoa majibu.
“Tena
nawaambia msikomalie suala hili kama vile ni la kufa na kupona, rais
atalifanyia kazi muda si mrefu,” alisema Salva.
Alisema taratibu za kumwajibisha Profesa Muhongo kama
kiongozi wa kisiasa hazifanani na hatua zilizochukuliwa kwa Katibu Mkuu wa
wizara hiyo, Maswi kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Serikali.
Akizungumzia ziara za Profesa Muhongo anazoendelea nazo
mikoani, Rweyemamu alisema tuhuma hizo hazimzuii kufanya kazi kwa kuwa bado
hajaondolewa kwenye nafasi ya uwaziri aliyonayo.
“Huyu
bado ni waziri, ana haki ya kuendelea na ziara zake kama kawaida, kumbukeni
wizara yake ina mambo mengi ambayo yanapaswa kusimamiwa kila siku,” alisema
Rweyemamu.
Desemba 22, mwaka jana, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa
Mkoa wa Dar es Salaam, alisema amemuweka kiporo Profesa Muhongo maana bado
hajapata ufafanuzi kuhusu mambo kadha wa kadha, na kwamba baada ya siku mbili,
tatu, atakapopata ufafanuzi na kujiridhisha, atachukua uamuzi.
Siku nne baadaye, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue,
alinukuliwa na vyombo vya habari akisema Rais Kikwete bado hajakamilisha
kulishughulikia suala hilo na kwamba litakapokuwa tayari wananchi watajulishwa
hatua alizochukua.
MISAMAHA YA KODI
Kuhusu misamaha ya kodi ambayo Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), imesema imeongezeka kutoka Sh trilioni 1.48 mwaka 2012/13 hadi
trilioni 1.82 mwaka 2013/14, ikiwa ni ongezeko la Sh bilioni 334, Rweyemamu
alisema wabunge ndio wanapaswa kulalamikiwa.
Alisema katika Bunge lililopita Serikali ilipeleka muswada
wa kufuta misamaha ya kodi, lakini wabunge hawakuupitisha.
Rweyemamu alisema bila kupitisha muswada huo na hatimaye uwe
sheria, suala hilo halitakwisha.
“Wabunge
wanapiga kelele kuhusu misamaha ya kodi wakati mwaka jana Serikali ilipeleka
muswada wa kufuta misamaha waliukataa na kuuchanachana…tunawaomba siku nyingine
wakipelekewa waupitishe.
“Sisi
hatupendi haya mambo na kama wanaonekana hawapendi, tunawashauri waupitishe ule
muswada ili tuondokane na tatizo hili,” alisema Rweyemamu
KURA YA MAONI
Katika hatua nyingine, Rweyemamu alikanusha taarifa
zinazoendelea kusambazwa kuwa Rais Kikwete alivunja sheria ya kura ya maoni
kutokana na kutopelekwa Katiba iliyopendekezwa kwenye Gazeti la Serikali.
“Hizi
taarifa si za kweli, Rais Kikwete alitimiza taratibu zote kulingana na matakwa
ya kura ya maoni, baada ya kupokea Katiba inayopendekezwa Oktoba 8, mwaka jana,
ilipofika Oktoba 10, ilitangazwa katika Gazeti la Serikali,” alisema
Rweyemamu.
Alisema hawana hofu kwa vile maandalizi ya kura ya maoni
yanaendelea vizuri.
Rweyemamu alisema nakala za Katiba inayopendekezwa
zitatolewa kwa ajili ya kutoa elimu japokuwa hazitawafikia watu wote kutokana
na wingi wa wananchi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “SAKATA LA ESCROW : IKULU YAELEZAHATIMA YA KIPORO CHA MUHONGO, YASEMA RAIS KIKWETE ATATIMIZA AHADI HIVI KARIBUNI.”
Post a Comment