Thursday, January 8, 2015

YAMETIMIA....WATUMISHI WA HALMASHAURI WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMLIPUA KWA BOMU MKURUGENZI WAO




WATU wanne wakazi wa wilaya ya Iramba, wakiwemo watumishi wawili wa halmashauri ya wilaya hiyo, wanashikiliwa na polisi mkoani Singida kwa tuhuma za kufanya jaribio la kutaka kumuua Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Iramba kwa bomu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Thobias Sedoyeka amethibitisha na kusema watu hao, ambao majina yao yamehifadhiwa kutokana na kutokukamilika uchunguzi wa polisi juu ya suala hilo, walikamatwa kwa nyakati na maeneo tofauti.

Kamanda Sedoyeka pia alisema ujumbe ambao alitumiwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Iramba, umekwishapelekwa kwa mtaalamu wa kung’amua miandiko ili kuweza kujua mtu aliyeuandika.

Alisema kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, ambaye mapema mwezi huu alinusurika kifo baada ya kitu kinachodhaniwa kuwa bomu kulipuka kitandani mwake, Halima Mpita (47), tayari amekwishahojiwa kuhusu ujumbe uliokuwemo kwenye bahasha.

Wakati huo huo, uchunguzi wa wataalamu wa kutegua mabomu kutoka JWTZ, unaonesha kuwa kitu kilicholipuka kitandani kwa Mkurugenzi Mtendaji huyo Januari 2, mwaka huu, halikuwa limetengenezwa kikamilifu kufikia hatua ya kuitwa bomu.

“Hii inatokana na mtengenezaji kutumia vitu viwili tu; yaani betri na kilipuzi badala ya kutumia vitu vitano”, alisema Sedoyeka, huku akiacha kutaja vitu vingine vitatu vinavyokamilisha utengenezaji huo".

Aliongeza kuwa, “hiyo ndio sababu iliyosababisha kifaa hicho kutoleta madhara makubwa”.

Siku hiyo ya tukio majira ya saa 1.15 asubuhi, Mkurugenzi huyo akiwa nyumbani kwake, akijiandaa kwenda kazini, alilipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu.

Siku mbili kabla ya mlipuko huo, Mkurugenzi huyo alipokea bahasha kutoka kwa katibu muhtasi wake majira ya saa 4.00 asubuhi na alipoifungua alikuta ujumbe usemao: ”Poleni sana, hatuwezi kufanya dili la milioni 90 halafu mkala peke yenu sisi mkatudhulumu tukawaacha”.

Na Abby Nkungu, Singida

0 Responses to “YAMETIMIA....WATUMISHI WA HALMASHAURI WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA KUMLIPUA KWA BOMU MKURUGENZI WAO ”

Post a Comment

More to Read