Thursday, February 5, 2015
HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE YA KUADHIMISHA SIKU YA SHERIA NCHINI, TAREHE 04 FEBRUARI, 2015 DAR ES SALAAM
Do you like this story?
Mheshimiwa
Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Tanzania;
Mheshimiwa
Anne Semamba Makinda, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa
Asha-Rose Migiro, Waziri wa Katiba na Sheria;
Waheshimiwa
Majaji wa Mahakama ya Rufani;
Mheshimiwa
Omar Othman Makungu, Jaji Mkuu wa Zanzibar;
Mheshimiwa
Shabani Ali Lila, Jaji Kiongozi;
Waheshimiwa
Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania;
Mheshimiwa
George Masaju, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ;
Waheshimiwa
Majaji Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa
Majaji wa Mahakama ya Rufani wastaafu;
Rais wa Chama
cha Mawakili Tanganyika;
Waheshimiwa
Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa;
Wasajili,
Wakurugenzi na Watendaji wa Mahakama;
Mahakimu na
Mawakili;
Mtendaji Mkuu
wa Mahakama;
Watumishi wa
Mahakama;
Wageni
waalikwa;
Mabibi na
Mabwana;
Nakushukuru
sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kwa mara nyingine tena kushirikiana
nanyi katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Tanzania. Hii ni mara yangu ya nane
na ya mwisho kuhudhuria sherehe hizi nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Sherehe za mwakani zitahudhuriwa na Rais mpya. Natumai mtaendelea
kumualika.
Napenda
kuwashukuru wale wote tulioshirikiana nao katika utekelezaji wa jukumu zito la
kuimarisha mhimili wa Mahakama katika kipindi changu cha uongozi.
Napenda kukutambua,
wewe mwenyewe Mheshimiwa Mohamed Chande Othman na Majaji Wakuu waliokutangulia,
Mheshimiwa Barnabas Samata niliyemkuta na Mheshimiwa Augustino Ramadhani
aliyemfuatia. Nawashukuru kwa ushirikiano wenu, umakini, weledi na umadhubuti
wa hali ya juu kwa kuwaongoza wenzenu vizuri katika kutoa haki nchini. Nyote
mlikuwa kielelezo kizuri cha utoaji haki hapa nchini na kioo cha uongozi bora
wa Mahakama yetu. Pamoja nanyi nawashukuru Majaji wote wa Mahakama ya Rufani na
wa Mahakama Kuu, Wasajili, Mahakimu Wakazi, Mahakamu wa Mahakama ya Mwanzo
ambao wote mmejitoa kusimamia utoaji wa haki katika nchi yetu. Vile vile,
namtambua Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Watendaji wa ngazi zote pamoja na
watumishi wote wa Mahakama kwa kazi yao nzuri waifanyayo.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Kauli mbiu ya
maadhimisho ya mwaka huu yaani, “Fursa ya Kupata Haki: Wajibu wa Serikali,
Mahakama na Wadau” ni muafaka kabisa kwa wakati uliopo. Inatoa fursa kwa
mihimili yetu miwili ya dola na wadau wengine kupima jinsi tunavyotimiza wajibu
wetu. Naomba tutumie fursa hii tuangalie yale tuliyofanya katika kipindi cha
miaka tisa (9) ya uongozi wangu kuhusu kuimarisha utoaji wa fursa ya kupata
haki nchini.
Kuboresha
utoaji wa haki na utawala wa sheria nchini ilikuwa miongoni mwa mambo
tuliyoyapa umuhimu wa juu katika majukumu ya Serikali yetu. Kwa ajili hiyo
tumejitahidi kutambua mahitaji na changamoto zilizokuwa zinaikabili Mahakama
nchini na kujaribu kutafuta majawabu. Tumechukua hatua na kufanya mambo
mbalimbali kwa madhumuni ya kuiwezesha Mahakama kutekeleza wajibu wake wa kutoa
haki.
Fursa ya
Kupata Haki
Mheshimiwa
Jaji Mkuu,
Kama
ulivyosema, wewe mwenyewe fursa ya kupata haki imegawanyika katika sehemu
mbili. Kwanza, ni fursa ya kuifikia Mahakama, na pili, ni fursa ya kunufaika na
huduma za Mahakama yaani kupata haki. Dhana hii inazilazimu Serikali na
Mahakama kufanya kazi kwa pamoja, kwani mhimili mmoja pekee hauwezi kufanikisha
haya yote mawili. Kimsingi, Serikali inao wajibu wa kuweka mazingira mazuri kwa
Mahakama kuweza kutimiza wajibu wake huo wa kutoa haki kwa wakati.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Ninapoiangalia
Mahakama ya leo ninafarijika kuona kwamba hatua zilizochukuliwa na Mahakama
yenyewe na nyingine zilizochukuliwa kwa kushirikiana na Serikali zimesaidia kuleta
mabadiliko kwenye mifumo na kuboresha utoaji wa haki. Changamoto za kimfumo
zilizokuwapo ziliathiri ufanisi katika utoaji haki nchini hususan zilisababisha
ucheleweshaji wa mashauri na hukumu.
Hali hii
imefanya utatuzi wa migogoro ya mikataba, biashara, ardhi, mahusiano kazini
kuchelewa sana (labor matters). Kwa ujumla, jitihada zetu za kukuza uchumi
zilipambana na vikwazo vya mifumo yetu ya sheria. Hali kadhalika, kwa upande wa
mifumo ya haki jinai, taratibu za kuendesha mashauri hazikuakisi mahitaji ya
kutoa haki kwa kuadhibu wakosaji kwa wakati na kutoa fidia na ahueni nyingine
inayofaa kwa wahanga wa uhalifu.
Mambo mengi
yamefanyika kuboresha Mahakama. Tumetunga Sheria namba 4 ya mwaka 2011 ya
uendeshaji Mahakama ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Mfuko wa Mahakama
na kuwezesha Mahakama kuwa na bajeti inayotabirika na ya uhakika. Fedha za
Mfuko huu zimekuwa zikiongezeka kutoka bilioni 57.8 mwaka 2012/2013 hadi
bilioni 89.6 mwaka 2014/15 sawa na ongezeko la asilimia 54.8. Katika mfumo huu
mpya tumeanza sasa kutenga bajeti ya maendeleo inayowezesha uwekezaji katika
upatikanaji wa miundombinu ya utoaji haki. Nimesikia mwaka huu bajeti ya
maendeleo haijaingia, naomba niwahakikishie kuwa mtaipata. Jana nilizungumza na
Waziri wa Fedha aliyenihakikishia kuwa katika nusu ya pili ya mwaka huu wa
fedha wataanza kutoa fedha.
Jambo lingine
muhimu tulilofanya lilikuwa ni kuongeza rasilimali watu. Tumepunguza uhaba
mkubwa uliokuwepo na kuwezesha Mahakama kuboresha kazi yake ya kutoa haki. Hivi
sasa kuna Majaji wa Rufani 16 kutoka 9 waliokuwepo mwaka 2005 na kuna Majaji wa
Mahakama Kuu 81 kutoka Majaji 35 waliokuwapo 2005. Ninafurahi kuwa kati ya
Majaji wote wa Mahakama ya Rufaa na Mahakama Kuu waliopo, Majaji 38 sawa na
asilimia 39.2 ni wanawake. Haya ni mageuzi makubwa. Natambua kuwa mahitaji
halisi ni kuwa na Majaji 120. Napenda kukuhakikishia Mheshimiwa Jaji Mkuu kuwa
mtakapokuwa tayari nileteeni mapendekezo yenu nifanye uteuzi. Kwa upande wa
Mahakimu Wakazi, hadi mwaka huu idadi yao ilifikia 677 nchi nzima ukilinganisha
na Mahakimu Wakazi 151 mwaka 2005. Mwaka wa jana pekee tulitoa kibali cha
kuajiri Mahakimu wapya 300.
Katika
kipindi hiki pia tulifanya mambo mawili mengine muhimu kwa utekelezaji mzuri wa
majukumu ya Mahakama. Kwanza ni lile la kukamilisha mchakato wa kutenganisha
shughuli za upelelezi na uendeshaji wa mashtaka. Imesaidia kupunguza
ucheleweshaji wa mashauri na kuimarisha utoaji wa haki.
Jambo la pili
ni kuanzishwa kwa nafasi ya Watendaji wa Mahakama iliyo waondolea Majaji
majukumu ya utawala na fedha na kuwaaacha washughulike na utoaji wa haki. Jambo
hili limeboresha na kuimarisha utendaji na uendeshaji wa shughuli katika
Mahakama kwa namna ambayo haijawahi kuwepo huko nyuma.
Huduma ya
Msaada wa Kisheria
Mheshimiwa
Jaji Mkuu,
Nakubaliana nawe
kuwa kukosekana kwa msaada wa kisheria kwa wale wasio na uwezo wa kulipia
huduma ya uwakili ni kikwazo kwa watu hao kupata fursa ya kupata haki. Pia
inakwaza utoaji wa haki. Nimefurahishwa na pendekezo lako la kuiomba Serikali
kuona uwezekano wa kugharamia huduma za uwakili kwa watuhumiwa wasio na uwezo
kifedha nje ya watuhumiwa wa makosa ya mauaji. Umeomba sasa tuangalie na wale
wenye makosa yenye adhabu kubwa na vifungo virefu. Nakubaliana nawe kuwa wakati
sasa umefika wa kuyaangalia mambo hayo kutokana na mabadiliko mbalimbali
yaliyotokea nchini ikiwemo kuongezeka kwa aina ya makosa, adhabu na kuwepo kwa
Wanasheria wa kutosha wa kuweza kutoa huduma hiyo ni jambo linalowezekana. Sisi
katika Serikali tutalifanyia kazi pendekezo hilo na tutawashirikisha mtupe
maoni yenu ya namna bora ya kutekeleza wazo hili. Naamini, tukifanya hivyo,
tutakuwa tumepanua fursa kwa watu wengi kupata haki ya kisheria.
Wajibu wa
Mahakama
Mheshimiwa
Jaji Mkuu,
Kama
nilivyosema awali, fursa ya kupata haki inategemea pia jinsi Mahakama
inavyotelekeza ipasavyo wajibu wake. Nafurahishwa sana na hatua ambazo Jaji
Mkuu umechukua ambazo zimewezesha kuboresha fursa ya kupata haki. Taarifa
uliyoitoa hapa leo imeonesha wazi mafanikio yaliyopatikana. Kufuatia uamuzi
wenu wa kujiwekea ukomo wa muda wa kuendesha kesi na idadi ya kesi kwa kila
Jaji na Hakimu, mmeweza kupunguza mashauri ya siku nyingi kwa asilimia 50
kutoka mashauri 6,887 mwaka 2012 hadi 3,632 katika Mahakama Kuu mwaka 2014.
Aidha, mmeweza kumaliza mashauri 52 kati ya 59 yanayohusu miradi mikubwa ya
serikali iliyoko katika Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Natoa rai kwa
wadau wengine wa sheria yaani waendesha mashtaka na vyombo vya upelelezi kwa
upande wa mashauri ya jinai pamoja na Mawakili wa kujitegemea kuunga mkono
juhudi zenu hizi. Bila shaka Mahakama itaendelea kuonyesha njia kwa kusimamia
mwenendo wa mashauri ya jinai na madai pasipo kuchelewesha. Ni matumaini yangu
kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka na vyombo vya upelelezi havitakuwa chanzo cha
kuchelewesha mashauri pasipo sababu za msingi.
Kusogeza
Huduma ya Mahakama karibu zaidi na Wananchi
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Natoa pongezi
nyingi kwamba kwa sababu ya mambo mbalimbali mazuri yaliyofanyika ambayo
yamesogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi. Sehemu kubwa ya migogoro
inayowagusa moja kwa moja wananchi imeshughulikiwa. Miongoni mwa hiyo ni ile ya
ardhi ambapo Mabaraza ya Ardhi yameundwa katika Kata zote nchini chini ya
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Jambo hili limepunguza sana
mzigo wa mashauri katika Mahakama zetu na kusaidia kuleta usuluhishi katika
jamii zetu. Inawezekana utendaji wa vyombo hivi una upungufu mbalimbali kinyume
cha matarajio ya wananchi. Dawa yake siyo kuvitelekeza bali kuyatambua matatizo
yaliyopo na kuyapatia ufumbuzi.
Wizara ya
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Halmashauri za Wilaya waendelee
kusimamia kwa karibu vyombo hivi muhimu kwa kusogeza huduma ya upatanishi na
kushughulikia migogoro midogo ya ardhi. Kuna malalamiko ya kutokuwepo kwa
Mabaraza ya Ardhi ya Wilaya katika Wilaya nyingi nchini. Kwa sababu hiyo watu
wamekuwa wanapata usumbufu katika kutafuta haki baada ya kutokuridhishwa na
uamuzi wa Mabaraza ya Kata. Wizara iharakishe kuunda Mabaraza hayo na
Halmashauri zisaidie upatikanaji wa majengo ya Mabaraza hayo.
Uhusiano wa
Mabaraza ya Ardhi na Mahakama Kuu
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Naambiwa kuwa
yapo malalamiko ya kukosekana mtiririko mzuri wa majalada kwenda Mahakama Kuu
Kitengo cha Ardhi. Nia njema ya kuanzisha Mabaraza ya Ardhi imezaa adha. Kilio kilichopo
ni kwamba Mabaraza hayo yamekuwa hayataki kutii amri ya Mahakama Kuu ya
kupeleka kumbukumbu pindi kunapokuwa na rufaa dhidi ya maamuzi yake ni jambo
ambalo sio tu halikutarajiwa bali halikubaliki. Linatia dosari katika utoaji wa
haki ya ardhi. Wakati huo huo, Wizara ya Ardhi iwachukulie hatua zipasazo
watendaji wa Mabaraza ya Ardhi wanaochelewesha kumbukumbu.
Ni matumaini
yangu kuwa wadau wanaohusika yaani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi, Wizara ya Katiba na Sheria na Mahakama mtakaa pamoja mapema
iwezekanavyo kulitafutia ufumbuzi tatizo hili. Kama itahitaji kupitia upya
sheria na taratibu ifanyike hivyo ili kuondoa kikwazo hiki na kuondoa
malalamiko yanayoendelea kwa muda mrefu sasa kuhusu jambo hili. Ipo rai kwamba
Sheria iwawajibishe watendaji wa Mabaraza ya Ardhi kwa Mahakama Kuu moja kwa
moja. Busara na hekima ya kufanya hivyo itafakariwe kwa makini. Ni matarajio
yangu kwamba hatua hizi zitachukuliwa mapema na pale kwenye mkwamo tuambiane
tuone namna ya kusaidia kukwamua.
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Nimefarijika
sana kusikia kwamba mkakati uliopo sasa ni kuongeza weledi kwenye Mahakama za
Mwanzo kwa kuendelea kuajiri wahitimu wa Shahada ya Sheria kwenye Mahakama
hizo. Hili ni jambo zuri ambalo litawawezesha Mawakili kusimamia na kuendesha
kesi kwenye Mahakama za Mwanzo. Madhali sasa, hatuna uhaba wa Wanasheria na
Mawakili, hili linawezekana. Uamuzi wetu wa kupanua huduma ya Mahakama Kuu kila
Mkoa ni mwendelezo wa dhamira yetu ya kuwafanya wananchi waweze kuifikia huduma
hiyo karibu na wanapoishi. Bado tunayo dhamira ya kukamilisha ujenzi wa
Mahakama Kuu kila mkoa ifikapo mwaka 2016 kama tulivyoagiza. Utekelezaji wa
dhamira hii unakwenda sambamba na uteuzi wa Majaji wengi wa Mahakama Kuu kama
nilivyoeleza awali.
Mapendekezo
yako, Mheshimiwa Jaji Mkuu, ya kupitia upya taratibu zilizopo ili kufanya
utatuzi wa migogoro na utoji haki uwe rahisi na unaoeleweka kwa wananchi ni
mzuri. Sehemu kubwa ya mashauri ya madai yanahusu usuluhishi.
Kinachotakiwa ni
kwa wanaosuluhishwa kuelewa na kuridhika na utaratibu uliotumika kusuluhisha
migogoro yao. Nakuomba, Mheshimiwa Jaji Mkuu na wenzako myafanyie kazi
mapendekezo hayo ili nchi yetu iwe na mfumo rahisi unaoeleweka wa kutatua
migogoro kwa haki, wepesi na haraka. Tukiweza kufikia lengo hili, wananchi
wataiona Mahakama ni chombo cha kutatua migogoro na siyo mahali pageni
pasipofaa kufika hata kama mtu hana budi kufanya hivyo. Hii itaondoa kishawishi
kwa wananchi kutafuta njia nyingine zisizofaa kupata haki zao. Tusikubali
tufike huko.
Hitimisho
Mheshimiwa
Jaji Mkuu;
Napenda
kumalizia hotuba yangu kwa kurudia kukushukuru kwa kunialika kuja kujumuika
nanyi siku hii adhimu. Katika kipindi hiki tumefanya mambo mengi yaliyoleta
mabadiliko madogo na makubwa katika mifumo ya utoaji wa haki nchini na kuongeza
ufanisi. Nawashukuru wale wote tulioshirikiana katika kuleta mabadiliko haya.
Busara za Majaji Wakuu watatu walioiongoza Mahakama, Majaji wa Rufani, Majaji
wa Mahakama Kuu, Wasajili, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama ni hazina
kubwa na ya kujivunia. Ushirikiano wa wadau mbalimbali umetusaidia kufikia hapa
tulipo sasa. Naamini kama watu wataendelea kuitumikia nchi yetu na watu wake
kwa moyo wa uzalendo na kujituma tutapiga hatua kubwa mbele.
Baada ya
kusema hayo yote naomba sasa niwatakie siku njema ya Sheria nchini.
Mungu Ibariki
Afrika!
Mungu Ibariki
Tanzania!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)


0 Responses to “HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA SHEREHE YA KUADHIMISHA SIKU YA SHERIA NCHINI, TAREHE 04 FEBRUARI, 2015 DAR ES SALAAM”
Post a Comment