Monday, April 13, 2015

KESHO USIKU WA ULAYA PATACHIMBIKA....




KESHO ni usiku wa ligi ya mabingwa barani ulaya ambapo mechi mbili za robo fainali zitashuhudiwa katika nchi za Hispania na Italia.

Dimba la Vicente Calderon, wenyeji Atletico Madrid watawakaribisha mahasimu wao wa mji, Real Madrid na mechi hiyo itachezeshwa na muamuzi Milorad Mazic kutoka Serbia.

Huko Italia, Juventus watachuana na Monaco ya Ufaransa, mechi zote mbili zitaanza majira ya saa tatu na  dakika arobaini na tano kwa saa za Afrika mashariki.

Atletico Madrid na Real Madrid zilizocheza fainali ya ligi ya mabingwa mwaka jana na kesho zitakutana kwa mara ya saba msimu huu, huku kila timu ikijipanga kulipa kisasi.

Mwezi mei mwaka jana mjini Lisbon, Ureno, Sergio Ramos alizima ndoto za Atletico kutwaa ubingwa wa kwanza wa ulaya kufuatia kusawazisha bao dakika za mwisho na kusababisha mechi ichezwe kwa dakika 120 na ndipo Real wakashinda 4-1.

Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa Atletico wameshinda mechi nne na kutoka sare mbili katika mechi sita walizokutana msimu huu.

Hii inajumuisha mechi mbili walizoshinda katika michuano ya Kombe la ligi na kombe la Mfalme.

Hata hivyo mwezi februari mwaka huu, Real Madrid walishushiwa kipigo cha mabao 4-0 katika mechi ya ligi kuu, La Liga na huo  ulikuwa ushindi mkubwa zaidi kwa mechi za mahasimu wa jiji la Madrid kwa miaka 28 iliyopita.

0 Responses to “KESHO USIKU WA ULAYA PATACHIMBIKA....”

Post a Comment

More to Read