Tuesday, September 15, 2015

TUNATAKA KAMPENI ZA AMANI NCHINI KOTE.




Tuanze makala haya kwa kumsifu Mungu, muumba wa vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana katika dunia hii. Hakika tumhimidi daima huku tukimuomba atuzidishie maarifa ya kutambua umoja wetu na amani katika taifa letu.
Hivi sasa vyama vya siasa vipo katika kampeni zao kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25.
Hili ni zoezi muhimu katika nchi zote zinazoheshimu misingi ya utawala bora na demokrasia.

Kampeni hizo zitakazohitimishwa Oktoba 24, mwaka huu ni muhimu kwa vile ndizo zinazotarajiwa kuwafanya wananchi wafanye uamuzi wa mgombea wa chama gani anafaa kutuongoza katika ngazi mbalimbali kuanzia udiwani, ubunge hadi urais.

Ni matarajio yangu kwamba wagombea nafasi mbalimbali watatumia nafasi hii ya kampeni kutangaza sera zao na mikakati waliyopanga ili kuwapa wananchi maendeleo wanayoyahitaji katika sehemu inayowahusu. Nimeamua kuandika haya kutokana na baadhi ya sehemu wafuasi wa vyama kuanza kupigana.

Huu siyo muda wa kupigana bali ni wakati mzuri wa vyama kunadi sera zao kama ambavyo zimeelezwa kupitia ilani zao na si wakati wa kutukanana au kumshambulia mtu badala ya kutangaza sera za chama.

Hatutaraji kuona vyama na wagombea wao wanatumia muda huu wa kampeni kupandikiza chuki na hamaki kwa wananchi ili kuwafarakanisha.

Wagombea wote wakumbuke kuwa mara baada ya uchaguzi kila Mtanzania anajua maisha yatakuwa yanaendelea.

Uchaguzi ni panga lenye makali sehemu zote mbili; kwamba unaweza kujenga taifa na unaweza pia kubomoa taifa letu.
Wagombea wakiruhusu sera na mikakati ndiyo iwe ajenda kuu, uchaguzi utamalizika kwa amani. Lakini wakiamua matusi, kashfa, uzushi na upandikizaji wa chuki kama ndiyo ajenda, taifa letu linaweza kujikuta pabaya.

Ndiyo maana nashauri kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamoja na vyama vya siasa na wadau wengine wa ulinzi na usalama wakutane mara kwa mara kabla ya uchaguzi ili wakubaliane katika mambo ya msingi kuelekea kwenye uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu.
Tunafahamu kuwa vyama vinafahamu kanuni na taratibu zote za uchaguzi.

Hata hivyo, kwa dalili ambazo tunaziona, uchaguzi huu hautakuwa wa kawaida kama chaguzi nyingine zilizopita.
Ni lazima viongozi wote wa vyama vya siasa na wagombea wote wakutane na kutoa tamko la kwamba kila mmoja atatimiza wajibu wake kwenye kuhakikisha kuwa amani na utulivu wa taifa letu unakuwa jambo la muhimu kuliko jambo lingine lolote.

Mimi pamoja na wafanyakazi wenzangu wa Kampuni ya Global Publishers, tunaahidi kwamba tutakuwa mstari wa mbele kuhakikisha uandishi wetu wakati wa kampeni za uchaguzi unalindwa na imani kwamba Tanzania Kwanza na mengine yatafuata baadaye.

Litakuwa ni jambo la kuhuzunisha akichomoza mgombea atakayehubiri utengano miongoni mwa wananchi. Nasisitiza amani tuliyonayo asiwepo wa kuiporomosha.Natoa wito, mgombea yeyote atakayepanda jukwaani na kuhubiri uchochezi, atengwe na asipewe kura kwa sababu huyo ni adui wa nchi bila kujali ametoka chama gani.

Ni lazima wagombea wote wajue kwamba amani katika nchi hii ikitoweka kuirudisha ni kazi kubwa sana na hata itakaporejea, mambo mengi yatakuwa yameharibika.Mifano ya nchi ambazo amani yao imeharibika na sasa wamebaki na majuto ni Somalia ambayo imebaki maghofu, Sudan Kusini, ambako wananchi hawana amani tena, Burundi wakati Pieree Nkurunziza (pichani) alipolazimisha kugombea urais, kabla ya uchaguzi wengi walijeruhiwa na wengine kufariki dunia.

Na katika nchi za Mashariki ya Kati, nchi za Kiarabu kama vile Syria wananchi wao wanakimbilia Ulaya na kupata mateso makubwa.Kwa hiyo jambo la kudumisha na kutangaza amani kwenye mikutano yetu ya kampeni ni jambo linalotakiwa kuwekewa kipaumbele cha hali ya juu.

Tunavitakia vyama vyote vitanavyoshiriki katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu kila la kheri katika kampeni zao, watambue kuwa amani ya nchi ni namba moja na vyama vyao ni baadaye na visiwe mbele ya Tanzania.

Watambue kwamba vyama vya siasa vinaweza kufa lakini Tanzania itabaki palepale ikibeba wananchi walio na vyama na wasio na vyama vya siasa.Kila mmoja wetu wakati tunaelekea kwenye uchaguzi mkuu kwenye moyo wake aseme; Tanzania Kwanza, vyama baadaye.


0 Responses to “TUNATAKA KAMPENI ZA AMANI NCHINI KOTE.”

Post a Comment

More to Read