Friday, September 18, 2015

MSAFARA WA SUGU WASHAMBULIWA KWA MAWE AKIELEKEA KATIKA KAMPENI ZAKE ZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA MBEYA


Gari la Mgombea Ubunge jimbo la Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi Sugu likiwa kituo cha Polisi kati jijini Mbeya mara baada ya kushambuliwa kwa mawe na watu wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa CCM

Sugu akiwa kituo cha Polisi na wafuasi wake.Picha Kenneth Ngelesi Mbeya .




Na Emanuel Kahema ,Mbeya
MGOMBEA ubunge  kupitia chadema jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi leo  amejikuta katika wakati mgumu baada ya msafara wake kushambuliwa na mawe na wafuasi wanaosadikiwa kuwa ni wa chama   cha mapinduzi CCM na kwamba katika tukio hilo watu wawili wamejeruhiwa akiwemo dereva aliyekuwa akimuendesha mgombea huyo  .

Tukio hilo la kushambuliwa kwa msafara huo, limetokea majira ya saa 11 za jioni katika eneo  la barabarani lililopo katika Kata ya Ghana mtaa wa Mbata jijini hapa  ambapo inasemekana mgombea huyo alikuwa  katika harakati za kampeni kuomba kura kwa wananchi wa Iziwa  ambapo mgombea huyo alikuwa ndani ya gari yake yenye namba za usajili T161 CPP Toyota  Land Cruser VX .

Awali, wafuasi wa chama cha mapinduzi CCM, walikuwa katika mkutano wa hadhara wa kumnadi mgombea wao ngazi ya Udiwani katika kata ya Ghana iliyopo ndani ya Jiji la Mbeya, hivyo wakiwa kwenye harakati hizo inasemekana walishangaa kuona msafara wa sugu ukipita katikati ya mkutano huo hivyo kushindwa kuvumilia na kuanza kurusha mawe huku wengine wakishikana mithili ya kutaka kupigana.

Katika vurugu hizo gari aliyokuwa amepanda mgombea huyo  lilipasuliwa kioo cha mbele na gari ya chama cha mapinduzi CCM wilaya ya Mbeya, ikipasuliwa kioo cha mbele .
Aidha Vurugu hizo zimesababisha   majeruhi wawili ambao wamelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Mbeya akiwemo dereva wa mbunge huyo na mfuasi mmoja wa chadema.

Kutokana na hali hiyo  mgombea huyo wa ubunge mbeya mjini kwa tiketi ya Chadema alilazimika kuikatisha zoezi lake la kuongea na wakazi wa Kata ya Iziwa iliyopo Jijini Mbeya kwa muda, kutokana na kulazimika kuripoti katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.

Mgombea huyo ilimlazimu kufika kituoni na kuchukuliwa maelezo na baada ya hapo aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa lakini gari yake yenye namba za usajili T161 CPP aliyokuwa akiitumia katika kampeni zake ikibaki polisi.


Hata hivyo, mgombea huyo alipomaliza kutoa maelezo  katika kituo cha polisi cha kati cha Wilaya ya Mbeya, aligoma kuzungumza na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa kwenye eneo la tukio na kuwataka wafike katika mkutano kwani ndipo atakapotolea ufafanuzi wa suala hilo hilo.


Mwisho.

0 Responses to “MSAFARA WA SUGU WASHAMBULIWA KWA MAWE AKIELEKEA KATIKA KAMPENI ZAKE ZA KUWANIA UBUNGE JIMBO LA MBEYA ”

Post a Comment

More to Read