Friday, August 15, 2014

WAZIRI MKUU PINDA ASISITIZA UMUHIMU WA ARDHI KATIKA UWEKEZAJI.




Na Eleuteri Mangi- MAELEZO
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda amewatoa Watanzania hofu kuhusu suala la wageni kumiliki ardhi nchini.

Waziri Mkuu Pinda alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es salaam wakati akifungua mkutano wa pili wa majadiliano ya pamoja kati ya Serikali ya Mitaa ya China na Tanzania ambapo walishirikiana pia na sekta ya biashara kutoka nchi hizo.

“Hofu ni halali na ni lazima kwa Watanzania katika masuala ya umiliki wa ardhi maana ni vema tuifikishe nchi mahali pazuri” alisema Pinda.
Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa Tanzania ni nchi inayolinda ardhi yake tofauti na nchi nyingine ambapo ardhi yote ni mali ya umma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio mwenye dhamana na mamlaka na ardhi ya Tanzania kwa niaba ya Watanzania.

Akifafanua Waziri Mkuu alisema kuwa suala la mwananchi au mwekezaji kumiliki ardhi hutolewa kwa kipindi kwa maalumu kwa minajili ya kutoa huduma mbalimbali za kijamii ambapo mwekezaji anapewa umiliki wa ardhi kwa muda tofauti kulingana na huduma anayotoa.

Waziri Mkuu Pinda alisema kuwa Watanzania ni lazima wajipange vizuri ili kuifikisha nchi mahali pazuri katika masuala ya uwekezaji ambapo nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
“Ushirikiano tunaoufungua na rafiki zetu kutoka China ni hatua kubwa ya kutambua na kusimamia dira yetu kati ya Tanzania na China ambayo ni kielelezo cha malengo makubwa ya mataifa haya mawili kwa kuzingatia uwekezaji unaojali usalama wa mazingira na kuboresha maisha ya watu” alisema Pinda.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia akimkaribisha Waziri Mkuu alisema kuwa sekta binafsi na uwekezaji nchini na China zinasaidia kuongeza fursa za biashara na uwekezaji baina ya nchi hizo mbili na zitasaidia kukuza kipato cha wananchi na nchi kwa ujumla.
 
Kwa upande wake Katibu Mkuu TAMISEMI Jumanne Sagini akitoa mada juu ya fursa za uwekezaji alisema kuwa Tanzania ina maeneo mengi yenye fursa za kiuwekezaji.
 
Sagini aliyataja maeneo hayo kuwa ni mikoa 8 ikijumuisha Tanga, Dar es salaam, Pwani, Morogoro, Mtwara, Lindi, Katavi na Singida.

0 Responses to “WAZIRI MKUU PINDA ASISITIZA UMUHIMU WA ARDHI KATIKA UWEKEZAJI.”

Post a Comment

More to Read