Friday, August 15, 2014
TANZANIA KUWA KITOVU KIKUU CHA MADINI YA VITO AFRIKA.
Do you like this story?
Na Greyson Mwase, Bagamoyo
Imeelezwa kuwa Tanzania
inatarajia kuwa kitovu kikuu cha madini ya vito barani Afrika baada ya
kubainika kuwa na utajiri mkubwa wa madini ya vito.
Hayo yalisemwa na mtaalamu wa madini ya vito na almasi kutoka Kitengo cha Uthamini wa Madini ya Vito na Almasi (TANSORT) kilicho chini ya Wizara ya Nishati na Madini Teddy Goliama kwenye semina iliyoshirikisha Makamishna Wasaidizi wa Madini wa Kanda, Afisa Madini Wakazi na Wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini inayoendelea mjini Bagamoyo
Goliama alisema Tanzania kupendekezwa kuwa kitovu kikuu cha madini ya tanzanite ni matunda ya ziara iliyofanywa na Kitengo cha TANSORT kwa kushirikisha wataalamu wa wizara ikiwa ni pamoja na ushiriki wake katika maonesho ya kimataifa ya vito ya Thailand yajulikanayo kama Bangkok Gem and Jewellery Fair
Alisema sababu zilizopelekea Tanzania kupendekezwa kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito Afrika ni kutokana na wingi na aina mbalimbali za madini hayo pamoja na madini hayo kupendwa na wafanyabiashara wengi kutoka Thailand na nchi nyinginezo duniani.
Alisema awali Waziri Mkuu wa Thailand aliitembelea nchi ya Tanzania na kukutana na Serikali pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Madini na kukubaliana maeneo ya kushirikiana ambapo aliahidi kuisaidia Tanzania katika kukuza biashara ya madini ya vito.
Goliama aliendelea kusema kuwa Waziri Mkuu huyo aliikaribisha Tanzania kutembelea Thailand pamoja na kukutana na wataalamu wa sekta wa madini wa nchi hiyo ambapo ujumbe wa wataalamu wa madini ukiongozwa na Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia madini Mh. Stephen Maselle ulitembelea nchi ya Thailand na kukutana na uongozi wa chama cha wafanyabishara wa madini Thailand unaoshirikiana na Serikali ya Thailand bega kwa bega.
Alisema kuwa moja ya mikakati ya kukuza biashara ya madini ya vito iliyowekwa ilikuwa ni kutoa fursa kwa nchi ya Tanzania kushiriki katika maonesho ya kimataifa ya Bangkok Gem and Jewellery Fair ambayo hufanyika mara mbili kwa mwaka, Februari na Septemba.
Alisisitiza kuwa mara baada ya Tanzania kufanya vizuri katika maonesho hayo na kubainika kuwa na hazina kubwa ya madini ya vito ilipendekezwa kuwa kitovu cha biashara ya madini hayo barani Afrika.
“ Mpaka sasa kwa bara la Afrika hakuna kituo cha biashara ya madini ya vito, maonesho ya Arusha Gem Fair yamekuwa yakitumika kama njia ya kuwakutanisha wafanyabiashara mbalimbali barani Afrika.’’ Alisisitiza Goliama
Aliendelea kusisitiza kuwa Tanzania imeweka mkakati wa kuboresha maonesho yao kuwa ya kimataifa zaidi barani Afrika na kukutanisha wafanyabiashara kutoka mabara mengine duniani pamoja na kuwa kituo kikuu cha madini barani Afrika.
Akizungumzia mchango wa biashara ya madini ya vito nchini Thailand, Goliama alisema kuwa biashara hiyo ni ya tatu katika kuchangia pato la nchi ya Thailand.
Wakati huo huo akizungumzia biashara ya madini ya vito inavyofanyika mtaalamu mwingine kutoka TANSORT Sanawa Matiko alisema kuwa biashara ya madini ya vito mara nyigi inafanyika kwenye maonesho ikihusisha kukutanisha wafanyabiashara yaani wauzaji na wanunuzi wa madini hayo.
“ Maonesho hayo hutumika kama njia moja wapo ya kujenga mtandao wa kibiashara pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji katika madini ya vito nchini’’ alisema Matiko
Matiko aliendelea kusema kuwa mara nyingi maonesho ya kimataifa hutumika kwa wafanyabishara kupata taarifa mpya (updates) za biashara ya madini ya vito pamoja na vifaa vya kisasa kwa ajili ya madini ya vito vilivyogunduliwa na taasisi zinazotengeneza vifaa hivyo.
Akizungumzia biashara ya madini kwa upande wa Tanzania Matiko alisema Tanzania inatakiwa kutumia heshima kubwa iliyopewa kwa kutangaza zaidi madini yake hususan ya vito ndani na nje ya nchi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “TANZANIA KUWA KITOVU KIKUU CHA MADINI YA VITO AFRIKA.”
Post a Comment