Tuesday, September 15, 2015
MAGUFULI; REKODI YAKE YA UCHAPAKAZI INAIBEBA CCM
Do you like this story?
Harakati
za uchaguzi nchini zipo katika kipindi muhimu cha kampeni ambapo mwaka huu wa
uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani, Watanzania wameamka zaidi kwa
kufuatilia na kusikiliza sera na vipaumbele vya wagombea mbalimbali wa nafasi
zote kutoka vyama vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi huo unaotarajiwa
kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Ukitazama uchaguzi huu utaona kuwa nafasi ya
urais ndiyo inayozungumziwa sana kwa sasa kwa kuwataja wagombea wawili wakubwa wanaochuana
vikali ambao ni Mhe. John Pombe Magufuli anayegombea kwa tiketi ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa anayegombea kwa tiketi ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambacho ni moja kati ya vyama vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Nguvu ya wawili hawa inapimwa na mambo mengi,
mengine ni ya kishabiki lakini mengine ni ya kimantiki zaidi kwa maana ya
rekodi zao kwa kipindi cha nyuma cha utumishi wao, kila mmoja akiwa serikalini.
Japokuwa ana historia ndefu ya kisiasa, wananchi
wengi walianza kumfahamu Lowassa mwaka 2005 alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wadhifa ambao hakudumu nao kwani miaka
michache baadaye alijiuzulu kwa tuhuma za ufisadi.
Kwa upande wa Magufuli, wengi walianza
kumfahamu mwaka 1995 akiwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Biharamulo
Mashariki (Chato) kabla ya baadaye kuwa waziri kamili wa wizara hiyo
aliyoitumikia kuanzia mwaka 2000 hadi 2005. Mwaka 2005- 2008 alikuwa Waziri wa
Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi huku akiendelea kuwa Mbunge wa Biharamulo
Mashariki.
Mwaka 2008 alihamishiwa Wizara ya Maendeleo
ya Mifugo na Uvuvi akiwa waziri kamili huku akiendelea na nafasi yake ya ubunge
hadi mwaka 2010 ambapo kuanzia mwaka huo hadi hivi sasa alirudishwa tena kwenye
Wizara ya Ujenzi.
Akiwa kote huko, Mhe. Magufuli aliweza
kujitengenezea sifa kubwa ya uchapakazi kuliko mawaziri wengi wa kipindi chake.
Sifa hiyo inatajwa kutokana na matukio kadhaa aliyoyafanya ambayo mpaka sasa
yamebakia ndani ya vichwa vya Watanzania.
Moja ya matukio yaliyobaki ndani ya vichwa
vya wengi ni lile la kukamatwa kwa meli ya Wachina ikiwa na tani 293 za samaki
waliokuwa wakivuliwa kwa siri kwenye Bahari ya Hindi mwaka 2009 wakati huo Mhe.
Magufuli akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.
Umaarufu wa sakata hilo ulisababisha samaki
waliokamatwa kupewa jina la Samaki wa Magufuli huku kupitia wizara yake,
serikali ikitangaza kuitaifisha meli na kugawa samaki hao wa taasisi mbalimbali
za umma.
Tukio hilo ambalo liliamsha sifa za
uchapakazi wa Mhe. Magufuli liliishia kwa kuachiwa kwa wafungwa hao 35 kwa amri
ya Mahakama Kuu mwaka 2014, wakati huo Mhe. Magufuli akiwa waziri wa ujenzi
ambapo akiwa huko aliwastaajabisha Watanzania baada ya kuwafukuza wafanyakazi
wa vituo vya mizani wapatao 400 baada ya kufanya ziara ya kushtukiza na kubaini
suala la rushwa iliyokithiri.
Mbali na tukio hilo, Mhe. Magufuli, akiwa
ndani ya wizara ya ujenzi amefanikiwa kukibeba chama chake kwa kujivunia idadi
ya madaraja na barabara nyingi zenye kiwango cha lami zilizojengwa na serikali
kupitia wizara hiyo huku yeye akiwa msimamizi mkuu asiyekaa ofisini pekee.
Kuna kipindi alilazimika kuwawajibisha
makandarasi wavivu waliokuwa hawakamilishi ujenzi katika muda uliopangwa na
wale wanaokamilisha kwa kiwango cha chini bila kusitasita.
Wapo wanaobeza kishabiki uwezo wa Mhe.
Magufuli kwa kumfananisha na wagombea wengine lakini kwa wale wanaotumia jicho
la tatu kumtazama mgombea huyu watagundua kuwa ni mtu mwenye karama ya kipekee
ya uongozi uliotukuka kwa kuwa mtu asiyependa majivuno, asiye na makundi,
mnyenyekevu na mchapakazi anayefuata kanuni na sheria bila kuyumbishwa
kirahisi.,
Utakumbuka sakata la bomoabomoa liliyoikumba
nyumba ya meneja wa TANROADS iliyokuwa Ubungo na jinsi alivyotaka kuigharimu
serikali kwa kutaka kubomoa jengo la Tanesco, Ubungo kwa kuwa limejengwa ndani
ya hifadhi ya barabara.
Sifa zake ni nyingi ambazo nikisema nizitaje
zote, kurasa hazitatosha lakini kwa kifupi, ipo wazi kwamba utendaji wake wa
kazi uliotukuka ndani ya serikali za awamu zote alizowahi kuzitumikia, ni
hazina nzuri kwa chama chake na yeye mwenyewe na kama Watanzania wataachana na
ushabiki usio na mantiki, watamchagua kuwa rais kwani anazo sifa na vigezo
vingi kuliko mgombea mwingine yeyote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAGUFULI; REKODI YAKE YA UCHAPAKAZI INAIBEBA CCM”
Post a Comment