Monday, September 14, 2015
BASATA YAWALIMA MENO WASANII WANAOIMBA NYIMBO ZENYE LUGHA CHAFU.
Do you like this story?
KATIKA siku za hivi karibuni kumeibuka wimbi la wasanii
kuvunja maadili, kukaidi adhabu na kutumia lugha chafu kwa makusudi katika kazi
za Sanaa hususan muziki hali ambayo imezua malalamiko, masikitiko na hofu kwa
jamii ambayo ni walaji wa kazi za Sanaa.
Lugha hiyo chafu ambayo inajidhihirisha kwa matusi ya wazi,
maneno ya uchochezi, kashfa, kejeli, dharau na udhalilishaji wa kada mbalimbali
za kijamii wakiwemo viongozi wa kitaifa inaonesha wazi kulenga katika kuigawa
jamii na kufifisha amani, upendo, uzalendo na ustaarabu tuliokuwa nao
watanzania.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa misingi ya Sanaa Duniani kote
kazi zote za Sanaa zinapaswa ziwe ni zenye kuonya, kuelimisha, kuadabisha,
kukosoa, kuburudisha, kuhamasisha na kuchochea maendeleo chanya katika jamii na
siyo kuigawa au kuivuruga jamii.
Ndiyo maana msanii anayefanya kazi zake kwa kuzingatia
misingi ya Sanaa anatambuliwa kuwa ni kioo cha jamii, kiongozi na pia ni
mwalimu wa yale yote yaliyo mema katika jamii inayomzunguka.
Kinyume na misingi hiyo ya Sanaa, baadhi ya Wasanii, studio
za kurekodia na kutengenezea muziki, vyombo vya habari vya kielektroniki na
mitandao ya kijamii ama kwa kutumiwa au kwa utashi wao binafsi wamekuwa
wakijihusisha na Sanaa zenye viashiria vya uchochezi na kuvunja misingi ya
weledi katika Sanaa hususan katika kipindi hiki cha kampeni na maandalizi ya
Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani.
Aidha, baadhi ya Wasanii wamekuwa wakitumiwa na baadhi ya
vyama vya Siasa au wagombea na kujikuta wakitumiwa vibaya na kuvunja misingi ya
Sanaa kwa faida za kisiasa. BASATA linapenda kutoa maagizo yafuatayo:
1.Wasanii wana haki zote za kikatiba na kidemokrasia
kushiriki shughuli za Siasa lakini wanawajibika kwa kiwango cha hali ya juu
kulinda misingi ya weledi, maadili, miiko na hadhi yao kama inavyofanyika
katika tasnia zingine.
2.Wasanii wanapaswa kutambua kwamba kuna maisha na Taifa
baada ya uchaguzi mkuu. Umoja wa kitaifa na umoja baina ya wasanii wa kada zote
za Sanaa ndiyo utakuwa msingi mkuu wa kuendelea kusukuma gurudumu la maendeleo
ya Sekta ya Sanaa na Taifa kwa ujumla pasipo kugawanyika katika misingi ya
itikadi za kisiasa
3.Wasanii wasitumie nafasi na umaarufu wao kuligawa taifa,
kukashifu viongozi wa kitaifa, kudharau mamlaka, vyama na makundi mbalimbali
katika jamii kwa kile kinachoitwa ushabiki wa kisiasa. Ieleweke kuwa Serikali
haitafumbia macho wale wote watakovunja sheria, kanuni na taratibu. Tukumbuke
kuwa hakuna mtu aliye juu ya sheria.
4.Ijulikane kuwa wasanii kama kundi muhimu katika kipindi
cha kampeni za kisiasa ni sawa na watu wengine wanaopewa kazi ili kutimiza
lengo lililokusudiwa. Wasanii wasitumiwe kama vyombo tofauti na watu wengine.
BASATA linatoa onyo kali kwa msanii yeyote atakayeendelea
kukaidi, kuvunja maadili na kusambaza kwa njia yoyote ile kazi ya Sanaa yenye
ukengeufu wa maadili.
BASATA linawatakia wasanii wote utekelezaji mwema wa maagizo
haya lakini kubwa kuliko yote kutambua kwamba tunatakiwa kujenga mshikamano,
umoja wa kitaifa na kustawisha amani tuliyonayo ambapo ikitoweka itaathiri
ufanisi wa Wasanii na kuirejesha itatugharimu sana.
Sanaa itumike kulinda amani, kujenga upendo, umoja wa
kitaifa na mshikamano baina ya makundi mbalimbali ya kijamii.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “ BASATA YAWALIMA MENO WASANII WANAOIMBA NYIMBO ZENYE LUGHA CHAFU.”
Post a Comment