Tuesday, April 14, 2015
MAHABUSU DAWA ZA KULEVYA WAGOMEA CHAKULA SEGEREA.
Do you like this story?
Jengo la
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
Mahabusu zaidi
ya 15 wa gereza la Segerea, jijini Dar es Salaam wanaokabiliwa na kesi za
kusafirisha na kuingiza dawa za kulevya nchini, wanadaiwa kugoma kula wakilalamikia
kusota gerezani kwa muda mrefu huku kesi zao zikiendeshwa muda mrefu bila
kumalizika.
Mahabusu hao
ambao waligoma kwa siku tano hadi jana wanalalamika kwamba, wamecheleweshewa
haki zao zaidi ya miaka minne tangu wafunguliwe mashitaka na Jamhuri.
Kwa mujibu wa
barua ya mahabusu hao ambayo NIPASHE imeiona, wanailalamikia Jamhuri kwa
kuwasotesha zaida ya miaka minne wakati kesi zao zilikuwa kwenye hatua ya
kusikilizwa ushahidi wa Jamhuri na utetezi katika Mahakama Kuu ya
Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Hata hivyo,
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) aliwafutia mashitaka na kuwafungulia upya
mashitaka yale yale katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es
Salaam.
Mbali na mgomo
wa kula, barua hiyo imeeleza kwamba, baadhi yao wamejishona midomo kwa sindano
na kwamba bwana jela wa gereza hilo anawatembezea mkong’oto ili
wasiendelee na mgomo huo.
Pamoja na mambo
mengine, watuhumiwa hao wanalalamika kwamba hawaruhusiwi kupelekewa chai,
sukari, majani ya chai, vitumbua, maandazi na vitu vingine kwa mahitaji
yao.
“Tumeamua
kugoma kula chakula, tumechoka kusota mahabusu zaidi ya miaka minne sasa kesi
zetu zilifikia hatua ya kufunga
ushahidi wa
Jamhuri na nyingine utetezi ... ajabu DPP amezifuta na kuturudisha nyuma
mahakama ya chini, tunateseka sana kukaa
ndani... ndugu
zetu wamepigwa marufuku kutuletea mahitaji mbalimbali muhimu bila sababu za
msingi,” ilieleza sehemu ya barua hiyo.
Aidha, barua
hiyo iliendelea kudai kwamba, Bwana Jela wa Segerea amewazuia watuhumiwa wote
wanaokabiliwa na tuhuma za dawa za kulevya wasikutane wala wasifanye
mawasiliano yoyote na kwamba ikitokea wakakutwa wanaongea,
wanashushiwa kipigo.
MSEMAJI WA
MAGEREZA
NIPASHE
ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Magereza nchini, Deodatus Kazinja, kuzungumzia
madai hayo, lakini alisema kwa sasa yuko kwenye mafunzo, hivyo hawezi
kuzungumza chochote.
“Niko kwenye
mafunzo, siwezi kuzungumzia suala hilo wasiliana na Mkuu wa Magereza wa mkoa,”
alisema Kazinja kwa njia ya simu.
MKUU WA
MAGEREZA DAR
Mkuu wa
Magereza Mkoa wa Dar es Salaam, ASP Joel Bukuku, alithibitisha kutokea kwa
mgomo huo, ingawa hakutaka kulielezwa kwa undani.
Aliliambia
NIPASHE jana kuwa kulikuwapo na jaribio la mgomo wa kula, lakini kwa sasa hali
imerejea kama kawaida baada ya kuzungumza nao Alhamisi iliyopita
alipokwenda katika gereza la Segerea kuwasikiliza.
Ifuatayo ni
sehemu ya mahojiano kwa njia ya simu kati ya NIPASHE na ASP Bukuku:
NIPASHE: Afande
habari za Jumapili, unazungumza na NIPASHE, kuna taarifa mahabusu wa kesi za
dawa za kulevya kule Segerea wamegoma kula siku ya tano leo (jana).
ASP Bukuku:
Nzuri, habari za kazi, mmmh sina taarifa hizo kama kuna mgomo, lakini ngoja
nicheki nitakujibu.
Baada ya nusu
saa mahojiano yaliendelea hivi:
NIPASHE: Afande
habari za muda vipi kuhusu taarifa za mrejesho za mgomo wa mahabusu?
ASP Bukuku:
Kiukweli hakuna mgomo, kwa sasa hali iko shwari kwa sababu nilikwenda kuongea
nao siku ya Alhamisi niliposikia wana jaribio la mgomo.
NIPASHE: Nini
hasa malalamiko yao mpaka wafanye jaribio la kugoma kula?.
ASP Bukuku:
Watuhumiwa hao wanalalamika kuhusu kesi zao kupangiwa tarehe za kuanza
kusikilizwa na wana muda mrefu wako mahabusu, nimewasihi watulie kwa
sababu wiki za sikukuu ofisi za serikali zilisimama kufanya kazi, kwa hiyo
tutalishughulikia suala lao wasitishe jaribio hilo kwa hiyo kifupi hakuna
mgomo ila walifanya jaribio kama nilivyokueleza.
Februari mwaka
huu DPP aliwafutia watuhumiwa zaidi ya saba wa kesi za dawa za kulevya na
kuzirejesha Mahakama ya Kisutu na baada ya kumalizika usikilizwaji wa
maelezo ya mashahidi, kesi hizo zinasubiri tarehe ya kusikilizwa Mahakama Kuu.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “MAHABUSU DAWA ZA KULEVYA WAGOMEA CHAKULA SEGEREA.”
Post a Comment