Thursday, May 14, 2015

OKWI AMKINGIA KIFUA DANNY SSERUNKUMA




MSHAMBULIAJI hatari wa Simba, Mganda, Emmanuel Anord Okwi amemtetea Mganda mwenzake Danny Sserunkuma akidai nyota huyo wa zamani wa Gor Mahia hajazoea mazingira ya soka la Tanzania.

Simba wametangaza kuwaacha wachezaji wake watatu wa kimataifa akiwemo Danny pamoja na ndugu yake Simon Sserunkuma na Joseph Owino, huku wakimuacha beki wa kati ambaye ni Mganda pia, Juuko Mursheed.

Sababu ya kuachwa kwa wachezaji hao ni kuonesha viwango visivyoridhisha mbele ya kocha mkuu, Mserbia Goran Kopunovic.

Lakini mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe jana alisema Simon ameomba kupewa muda zaidi wa miezi sita (6) ili kuonesha kiwango chake na kama atashindwa basi atakubali kuvunjiwa mkataba.

Akizungumza na mtandao huu, Okwi amesema: "Danny (Sserunkuma) ni mfungaji mzuri, kamwe sijawahi kuwa na shaka juu ya hilo, alipokuwa Kenya alifunga magoli mengi, lakini hapa Tanzania hana bahati, mimi naona sababu kubwa ni kushindwa kuzoea kwa haraka soka la Tanzania".

"Danny hajawazoea wachezaji wa Tanzania na aina ya uchezaji wao, lakini kama angepewa muda na kuaminiwa na mashabiki pamoja na viongozi, naamini angeibuka kinara msimu ujao".

0 Responses to “OKWI AMKINGIA KIFUA DANNY SSERUNKUMA”

Post a Comment

More to Read