Wednesday, July 8, 2015

JK AHIMIZA WATANZANIA KUJIANDIKISHA BVR.




RAIS Jakaya Kikwete amewataka Watanzania kujiandikisha, vinginevyo wasije kushangaa watakapochaguliwa viongozi wasiofaa.

Wakati lengo la awali la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) lilikuwa ni kuandikisha Watanzania kati ya milioni 22 na milioni 23, hadi juzi taarifa za tume zinasema Watanzania 11,248,194 walikuwa wamean dikishwa.

Rais Kikwete alikuwa miongoni mwa wananchi wa Kata ya Msoga mkoani Pwani, waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kkura kwa mfumo mpya Biometric Voters (BVR), jana.

Akiwa ameongozana na mtoto wake, Ridhiwani ( Mbunge wa Chalinze) ambaye pia alijiandikisha, ilimchukua Rais Kikwete dakika 15 tangu kufika kwenye kituo na kukamilisha mchakato wa kujiandikisha na kupewa kitambulisho chake.
Baada ya kuwasili Kikwete alikwenda kujaza fomu namba moja, ambayo alitakiwa kueleza taarifa zake binafsi na anwani yake, kabla ya kwenda hatua ya pili ya kuchukuliwa alama za vidole 10 na kupigwa picha.

Akizungumza baada ya kukamilisha mchakato huo kwenye Kituo cha Hospitali kilichopo Kata ya Msoga, Kikwete alisisitiza wananchi kujiandikisha watimize haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi.

“Nitoe mwito kwa Watanzania kujitokeza kujiandikisha ili mtimize haki yenu ya msingi ya kumchagua kiongozi anayefaa na mnayemtaka, mchague rais, mbunge na diwani aliyewaridhia.

Msipojiandikisha msije sema, hee hata fulani kachaguliwa,” alisema. Alisisitiza, “sasa kama hutaki kupata haki ya kuchaguliwa basi timiza haki yako ya kikatiba ya kuchagua.”
Aridhishwa na uandikishaji Kikwete aliipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kazi nzuri na ya kuridhisha ya kuandikisha watanzania kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura licha ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.

“ Najua changamoto za mwanzo zilizowakabili, niwapongeze kwa hatua nzuri ambayo tume mmefikia, natambua na kuthamini kazi mliyoifanya mpaka sasa na mnayoendela kuifanya, hata kuna maneno yanasemwa semwa, msihofu ili mradi mna dhamira ya kweli ya kutekeleza kazi hii,” alisema.

Awali, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema mpaka sasa mikoa 13 imeshakamilisha kazi ya kuandikisha Watanzania kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Alisema hadi juzi, Watanzania 11,248,194 walikuwa wameandikishwa. Uandikishaji Dar Lubuva alisema wanaendelea na mchakato wa kuandikisha watanzania wenye sifa kwenye mikoa 11.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, kazi itaanza Julai 16 na Zanzibar wataanza Julai 13 mwaka huu. “Kwa sababu huu ni mfumo mpya, ulikuwa na changamoto zake, lakini mpaka sasa tunaendelea vizuri na lengo letu la awali lilikuwa ni kuandikisha Watanzania kati ya milioni 22 na 23, na kwa hali tunayoenda nayo, tuna imani tutafikia malengo tuliyojiwekea,” alisema Lubuva.

Alisema lengo la NEC ni kuhakikisha kazi ya kuandikisha ikafikia tamati katika mikoa ya Dar es Salaam na Zanzibar wiki ya pili ya Agosti.

Akizungumzia mkoa wa Pwani ambao uandikishaji ulianza jana, Lubuva alisema vipo vituo 1,752 na wameweka mashine za BVR 932. Lengo ni kutumia mwezi mmoja kukamilisha kazi hiyo kwa mkoa huo.

Lubuva alisisitiza kuwa NEC haitaacha kumwandikisha Mtanzania ambaye atakuwa amefika kituoni siku ya mwisho ya uandikishaji. HABARI LEO

0 Responses to “ JK AHIMIZA WATANZANIA KUJIANDIKISHA BVR.”

Post a Comment

More to Read