Saturday, October 10, 2015
NEC: VIFAA BVR FEKI
Do you like this story?
Mkurugenzi wa NEC, Ramadhani Kailima. |
Siku
moja baada ya kunaswa mashine zilizosadikiwa kuwa ni za uandikishaji wapiga
kura kwa njia ya kielektroniki (BVR), zilizokuwa zikiandikisha wafanyakazi wa
Kiwanda cha MM Steel jijini Dar es Salaam, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imeibuka na kueleza kuwa mashine hizo ni 'feki' na wala hazihusiani kwa namna
yoyote na vifaa vyao.
Mkurugenzi wa
NEC, Ramadhani Kailima, ndiye aliyetoa ufafanuzi huo wakati akizungumza na
Nipashe jana kuhusiana na mashine hizo ambazo zilikamatwa juzi wakati
zikiendelea kutumiwa kwa shughuli ya uandikishaji wa wafanyakazi wa kiwanda
hicho kilichopo katika eneo la Mikocheni.
Wakati Polisi
wakizikamata jana kwa ushirikiano na maofisa kadhaa wa NEC, tayari mashine hizo
zinavyofanana na BVR zilishaandikisha wafanyakazi zaidi ya 100 wa Kiwanda cha
MM Steel.
Akielezea zaidi
kuhusiana na tukio hilo, Kailima alisema kuwa, mara baada ya kupata taarifa za
kuwapo kwa mashine hizo, walienda kuzikagua na kubaini kuwa hazina uhusiano na
zile za Biometric Voter Registation (BVR), zilizotumiwa na wao (NEC)
kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
“Hakuna ukweli
wowote kuwa zile ni mashine za BVR na tumebaini ni feki, tena ni sawa na zile
zinazotumika kwenye ofisi mbalimbali kuandikisha wafanyakazi wake... hawa
waliosema ni mashine za kuandikishia wapiga kura hawako sahihi... si kweli,”
alisema Kailima.
Alisema endapo
watu wataendelea kuwa na shaka juu ya namna NEC inavyofanya kazi kwa sababu tu
ya kuona mashine kama hizo, basi wanaweza pia kukamata mashine za ofisi nyingi
zikiwamo za kwenye viwanja vya ndege, hospitali na hata manispaa kama ya
Kinondoni ambayo hutumia mashine kama hizo kwa shughuli zake mbalimbali.
“Mashine
tulizozikuta kwenye hiyo ofisi jana (juzi) ni computer mpakato (laptop) na
mashine za kuchukua alama za vidole. Hata wale wafanyakazi tulipowahoji
walibainisha kuwa wanazitumia kuorodhesha wafanyakazi wao kwa ajili ya usalama
wa ofisi... na tena zipo ofisi nyingi zinatumia mashine hizo,” alisema Kailima.
Kailima alitoa
tahadhari kwa wataalamu wanaovishauri vyama vya siasa kuwa makini na kuacha
kupotosha kwa kuwaleza mambo yasiyo na ukweli, hasa kuhusiana na NEC kwani wao
wanafanya kazi zao kisayansi zaidi na hakuna fursa ya kuwapo kwa ubabaishaji wa
aina yoyote.
Aliongeza kuwa
hawafanyi kazi zao kwa misikumo ya kisiasa, bali huzingatia utaalamu na hivyo
wanaotumiwa kwa ushauri na vyama waache kuwadanganya wanasiasa.
“Hawa wanasiasa
wanadanganywa na watu wanaojiita wataalamu... mashine hizi (zilizokamatwa)
hazihusiani na BVR," alisisitiza.
CHADEMA
WAHUSISHWA UCHUNGUZI
Akieleza zaidi
juu ya hatua walizochukua baada ya tukio la juzi, Kailima alisema kuwa (jana)
walifanya uchunguzi wa mashine hizo kwa kushirikiana na wawakilishi kutoka
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambao ndiyo walitoa malalamiko kwao
kuhusiana na madai ya kuwapo kwa mashine kama BVR zinazotumiwa kuandikisha
watu.
“Wataalamu wao
(Chadema) walikuja na tukathibitisha (wote) zile ni feki na hazihusiani kabisa
na mashine zetu za BVR,” alisema Kailima.
Kwa upande
wake, Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) John
Mnyika, aliitaka NEC ivikabidhi vyama vya siasa nakala za daftari la kudumu la
wapiga kura ili kuepukana na njama za wizi wa kura alizodai zinaweza kufanywa
na chama tawala -- Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumia
tukio la juzi kuhusu kukamatwa kwa vifaa vinavyofanana na mashine za BVR,
Mnyika alisema suala hilo walilikabidhi kwa maofisa wa NEC na Jeshi la Polisi
ambao wanalichunguza kwa kushirikiana na maofisa wa Chadema ili kubaini ukweli.
Kadhalika,
Mnyika aliitaka NEC kushughulikia suala hilo haraka na kutishia kuwa wasipotoa
majibu ya kina ndani ya siku tatu, atashauri wanachama wenzake kuishinikiza
ifanye hivyo ili kuondoa shaka iliyopo.
Hata hivyo,
Mnyika aliyasema hayo kabla ya kutolewa kwa maelezo ya Kailima kuhusiana na
uchunguzi walioufanya kwa mashine hizo zilizokamatwa Mikocheni.
Juzi, Chadema
walipata taarifa kutoka vyanzo vyao vyao kuwa kuna mashine zinazofanana na BVR
zinaandikisha watu na hivyo wakashirikiana na Polisi na NEC kuvikamata kabla ya
kwenda kuvichunguza. Meneja Mawasiliano wa MM Steel, Aboubakar Mlawa, alieleza
kuwa kampuni yao imeamua kuandikisha wafanyakazi wao kwa nia ya kudhibiti
usalama vitendo vya wizi, na kwamba tayari walishaandikisha wafanyakazi zaidi
ya 100 kati ya 900 waliokuwa wakitarajiwa kutoka kwenye viwanda vyao saba.
CHANZO: NIPASHE
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 Responses to “NEC: VIFAA BVR FEKI”
Post a Comment