Friday, October 9, 2015

KIJIJI CHA MAGIGIWE WILAYANI MBARALI CHENYE WAKAZI ZAIDI YA 900 HAKINA SHULE WALA ZAHANATI.




Kijiji cha Magigiwe kilichopo kata ya Miombweni wilayani Mbarali hakijawahi kuwa na shule wala zahanati tangu kianzishwe,hali ambayo inasababisha watoto wanaoishi kijijini hapo kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa saba kwenda katika shule ya jirani ya Mapogoro kupata elimu.

Kijiji hicho cha Magigiwe chenye wakazi zaidi ya 900,wengi wao wakiwa ni jamii ya wafugaji,hakijawahi kuwa na shule ya msingi wala zahanati,changamoto ambayo imeibuliwa na mfuko wa maendeleo ya jamii wa TASAF awamu ya tatu ambao umeamua kuwapelekea mradi wa ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa,mradi ambao umepokewa kwa furaha na wananchi hao ambao nao wameamua kujitolea nguvu zao ili kufanikisha ujenzi huo.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya mbarali,Venant Komba amewapongeza wakazi wa kijiji hicho kwa kujitolea kushiriki katika ujenzi wa shule hiyo, huku mratibu wa TASAF wilaya ya Mbarali,Amos Chiwaya akisema kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa miradi ya TASAF awamu ya tatu yenye maeneo manne ya utekelezaji.

Mkuu wa wilaya ya mbarali,Gulam Hussein kifu ametembelea kijiji hicho na kushiriki katika shughuli za ujenzi wa shule hiyo,huku akiwataka wananchi hao kuongeza bidii ili mradi huo ukamilike kwa wakati na hatimaye waweze kuletewa mradi mwingine wa zahanati.

0 Responses to “KIJIJI CHA MAGIGIWE WILAYANI MBARALI CHENYE WAKAZI ZAIDI YA 900 HAKINA SHULE WALA ZAHANATI.”

Post a Comment

More to Read