Thursday, November 5, 2015

WANAFUNZI SITA WA KIDATO CHA NNE MBEYA WAZUIWA KUFANYA MTIHANI WA TAIFA




Wanafunzi sita wa kidato cha nne katika shule ya sekondari Lupeta jijini Mbeya wameiomba serikali kuingilia kati hatma yao kielimu baada mwalimu mkuu wa shule hiyo kuwazuia kufanya mtihani wao wa kidato cha nne licha ya wanafunzi hao kukamilisha taratibu zote na kupata usajili wa baraza la mitihani la taifa, NECTA.

Wanafunzi hao ambao wanadai kutolewa ndani ya chumba cha mtihani na mwalimu mkuu wa shule yao, wamesema wanasikitishwa kuzuiwa kufanya mtihani wao wa mwisho jambo ambalo wamedai linawaharibia maisha yao, hivyo kuiomba serikali kuingilia kati.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo ambaye baada ya kusikia uwepo wa wanahabari shuleni hapo alifunga ofisi na kuondoka huku akizima simu yake ya kiganjani na ndipo ITV ikafika katika ofisi ya afisa mtendaji wa kata ya Iyunga, Diaz Mzee ambaye amedai kuwa ameambiwa na mwalimu mkuu huyo kuwa wanafunzi hao walishapewa barua za kufukuzwa shule hivyo hawana sifa ya kufanya mtihani wa taifa.

Wazazi na walezi wa wanafunzi hao ambao baadhi yao ni masikini wasiojiweza wamedai kuwa uongozi wa shule haujawatendea haki watoto hao na kuomba ngazi za juu za serikali kuingilia kati kuwasaidia vijana hao kupata haki yao.

0 Responses to “WANAFUNZI SITA WA KIDATO CHA NNE MBEYA WAZUIWA KUFANYA MTIHANI WA TAIFA ”

Post a Comment

More to Read