Wednesday, December 23, 2015
SAMUEL SITTA ASHINDWA KUJIZUIA, AAMUA KUACHANA NA SIASA
Do you like this story?
Kwa mara ya
kwanza tangu Kamati Kuu ya CCM ilipomuengua kwenye kinyang’anyiro cha uspika,
Samuel Sita ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, jana ameweka bayana
mustakabali wake; ameamua kustaafu siasa.
Sitta aliongoza
kwa mafanikio Bunge la Tisa kiasi cha kumfanya apewe kirahisi uenyekiti wa
Bunge la Katiba na hivyo kujijengea jina miongoni mwa wana-CCM kiasi cha
kujitumbukiza kwenye mbio za urais na baadaye kutaka kurudi tena kuliongoza
Bunge la Kumi na Moja.
Lakini
hakufanikiwa kupitishwa kuwania urais wala kugombea uspika, ambao aliahidi kuwa
angeengulkiwa angefika hata mahakamani.
Lakini jana
alikuwa na kauli tofauti.
“Mambo ya siasa
kwa sasa basi,” alisema Sitta alipoulizwa na kuhusu mipango yake ya baadaye
baada ya kutopitishwa na CCM kuwania uspika.
Sitta ambaye
amewahi kuongoza wizara mbalimbali, alisema kwa sasa anajikita katika uandishi
wa vitabu na kwamba kwa umri alionao na utumishi wake serikalini, umefika
wakati kwake kupumzika na kutoa ushauri wa masuala mbalimbali kwa wale
watakaohitaji mchango wake.
Novemba 15,
Kamati Kuu ya CCM ilimtosa Sitta na wengine waliojitokeza kuwania uspika na
badala yake ikateua majina matatu kwa ajili ya kupigiwa kura na wabunge wa CCM,
ambao walimchagua mbunge wa Kongwa, Job Ndugai kuwa Spika.
Kuenguliwa kwa
Sitta kulikuwa ni pigo lake la pili katika nafasi ya hiyo baada ya kukatwa na
kikao hicho mwaka 2010 alipokuwa akitetea nafasi yake. Wakati huo Anne Makinda
alichaguliwa kuongoza Bunge la Kumi lililomaliza muda wake mwaka huu.
Sitta
alijizolea sifa wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia mwaka 2005 hadi
2010, baada ya kuliongoza kuibua mijadala mbalimbali dhidi ya Serikali na
kashfa ya Richmond iliyomfanya Edward Lowasa kujiuzulu uwaziri mkuu.
Baada
ya kung’atuka
Alipoulizwa
atajishughulisha na nini baada ya kustaafu, Sitta ambaye pia alikuwa mwenyekiti
wa Bunge Maalumu la Katiba alisema: “Nipo tu nyumbani nimepumzika. Naridhika na
niliyoyafanya kwa Taifa. Wale watakaotaka kupata ushauri wakinifuata
nitawasikiliza.”
Alisema kwa
sasa anaandika makala ambazo baadaye ataziweka katika kitabu chake
kitakachoeleza hali ya nchi na historia za masuala mbalimbali.
“Ninachokiandika
ni mtazamo wangu binafsi, ni jinsi ambavyo mimi ninaona kwa macho yangu,”
alisema.
Alipoulizwa
kama atakubali kuongoza wizara iwapo Rais John Magufuli atamteua kuwa mbunge na
kisha waziri alisema: “Tusizungumze jambo ambalo halina mwelekeo huo.”
Hata hivyo,
alisema kwa mtazamo wake hadhani kama anaweza kufikiriwa kuwamo katika baraza
hilo.
Kupinga
uspika kortini
Kuhusu sakata
la uspika, Sitta alisema angekwenda mahakamani kupinga kuondolewa kwake, kama
tu mchakato wa chama hicho ungefanyika bila kufuata taratibu na watu kuonewa.
Katika
mazungumzo yake na Radio Uhuru FM wakati wa mchakato wa uspika, Sitta alisema
kutokana na hali ya joto la kisiasa ilivyo, ambayo ilidhihirika zaidi wakati wa
uchaguzi, wabunge walioshinda ni vijana na ni wazi spika anayehitajika ni
mwenye uzoefu.
Alisema licha
ya kwamba wapo waliojaribu kumshawishi asigombee nafasi hiyo tena, badala yake
awe anatoa ushauri pale inapobidi, alisisitiza bado ana wito wa kuwatumikia
wananchi kwa njia hiyo.
“Niliposema
(nitakwenda mahakamani) kama nisipoteuliwa na CCM kuwania uspika nililenga kama
kitatokea kitu kama uonevu. Yaani kama vingeletwa vigezo ambavyo havipo katika
mchakato,” alisema.
“Kama
unakumbuka mwaka 2010 kililetwa kigezo cha ‘spika mwanamke’. Hicho ndicho kitu
ambacho nilikilenga kwamba kikijitokeza sitakikubali. Uzuri ni kuwa hakikuwapo
na kumbuka kuwa jambo lile (la kupitishwa kuwania uspika) lilikuwa ni uamuzi wa
chama si mtu,” alisema Sitta.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
.gif)


0 Responses to “SAMUEL SITTA ASHINDWA KUJIZUIA, AAMUA KUACHANA NA SIASA”
Post a Comment