Wednesday, May 18, 2016

WAZEE WA MBEYA WAMPA TANO MAGUFULI.




UMOJA wa Wazee wa chama cha Mapinduzi (CCM), jijini Mbeya umepongeza jitihada zinazofanywa na rais Dr John Pombe Magufuli za kupambana na rushwa, ukwepaji wa kodi na ubadhirifu wa mali za umma kwa lengo la kuwaletea maendeleo Wananchi.

Tamko la Pongezi lilitolewa  na mwenyekiti wa Umoja huo Isakwisa Mwambulukutu wakati akizungumza na Waandishi wa habari pamoja na Wazee wa CCM wa jiji la Mbeya.

Alisema kitendo cha rais Magufuli kutumbua majibu kwa viongozi wasiofuata maadili ya utumishi kinawakumbusha wazee hao enzi za Waziri mkuu wa serikali ya awamu ya kwanza Hayati Edward Sokoine jinsi alivyopamba na wahujumu uchumi.

Alisema kasi ya rais Magufuli  itasaidia kuimarisha nidhamu na uwajibikaji sehemu za kazi kwa watumishi wa umma  kwa kutanguliza mbele maslahi ya umma na kufikia matarajio ya Watanzania ya kupata maisha bora.

“Watumishi umma walifikia mahali ambapo walifanya kazi kwa kadri ya matakwa yao bila kujali taratibu na kanuni za kazi, walisahau ile kauli aliyoitoa rais wa awamu ya pili Ally Hassani Mwinyi isemayo ‘usipowajibika ole wako, utakumbana na fagio la Chuma’ sisi tunaamini Magufuli ni fagio la Chuma.” Alisema

Aidha, Mwambulukutu alisema Taifa la Tanzania linaweza kuondokana na umasikini ikiwa Wananchi wataungana na rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha wanaleta Maendeleo ya Taifa.

“Ni ukweli usiopingika kuwa maendeleo ya mtu au taifa kwa ujumla hayawezi kupatikana kama watu hawataki kufanya kazi, tunampongeza kwa kuhimiza hilo na tunamwomba alisimamie kwa nguvu zote ili nchi yetu iweze kujikwamua kutokana na lindi la Umasikini.” Alisema.
Baadhi ya Wazee  John Mushi na Salome Mwaipasi  walisema matarajio yao katika serikali ya awamu ya Tano ni kuona wanaboreshewa huduma za afya.

Walisema kuwa kwa sasa wanalazimika kulipia vipimo na dawa  pindi wanapougua hivyo wamemuomba rais Magufuli kuwasaidia ili waweze kupata huduma hiyo bure.

“Tunategemea tutapata vipimo na madawa bure Hospitalini, taifa litakuwa na wasomi wengi kutokana na mfumo wake wa utoaji elimu bure, hivyo kutakuwa na mwamko mkubwa wa wazazi kuwapeleka watoto shule.” Alisema Mushi.
MWISHO

0 Responses to “WAZEE WA MBEYA WAMPA TANO MAGUFULI.”

Post a Comment

More to Read