Tuesday, July 12, 2016

RAIS MAGUFULI AAGIZA VYOMBO VYA SERIKALI KUANZA KUTUMIA MACHINE ZA EFD




Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dk John Pombe Magufuli amewaagiza makatibu wakuu kuhakikisha vyombo vyote vinavyokusanya mapato serikalini vinatumia mashine za kielekrtoniki (EFD).

Rais Magufuli ameyasema hayo wakati akizungumza na wakurugenzi wateule wa Halmashauri,Wilaya,Majiji na Manispaa Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kiapo cha ahadi ya uadilifu kwa viongozi hao wa umma.

“Vyombo vya Serikali lazima vianze kutumia mashine za EFD,haiwezekani  wafanyabiashara wawe na mashine za EFD alafu maafisa wa serikali hawana,kama tumeamua kwenda kwa elektroniki lazima twende hivyo”Alisema Rais Magufuli.

Aidha amewataka wakurugenzi  wote kuchukua mashine hizi na kwenda nazo katika maeneo yao ya kazi ili ziwasaidie katika ukusanyaji wa mapato ya serikali katika halmshauri zao.

Pia amewaagiza wakurugenzi hao kukusanya kodi na kutatua kero za wananchi wa chini zisizokuwa na lazima na kuongezea kuwa kama watakuta watendaji wa chini yao wasioendana  na kasi ya awamu ya tano basi watumie madaraka yao kuwaweka sawa.

Rais magufuli pia amewaagiza wakurugenzi hao kusimamia ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi kwakuwa waliahidi kutatua kero za wananchi na wahakikishe wanazitatua ili wananchi waishi vizuri kwa amani ndani ya nchi yao na kuongezea kuwa viongozi wa juu wana imani kubwa sana nao ndio maana hata wakachaguliwa kutoka katika watanzania hawa milioni 50.

Aidha Rais magufuli amewataka wakurugenzi hao kusimamia kuanzishwa kwa viwanda vidogo vidogo katika maeneo yao ili kukamilisha azma ya serikali ya awamu ya tano ya kuwa na viwanda.

Mbali na hayo pia amewataka wakurugenzi hao kubadilika kifikra na kuachana na kuongoza kwa historia kwani wananchi wa sasa wamebadilika na hivyo wafanye kazi kwa bidii ili kuwatimizia wananchi yale wanayotaka na hivyo nchi itasonga mbele.

0 Responses to “ RAIS MAGUFULI AAGIZA VYOMBO VYA SERIKALI KUANZA KUTUMIA MACHINE ZA EFD”

Post a Comment

More to Read