Friday, July 15, 2016

VIDEO:WAZIRI NAPE AFANYA MSAKO WA FILAMU ZISIZO NA STIKA ZA TRA KARIAKOO


Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye( kushoto) akiangalia bidhaa za filamu na muziki zilizokamatwa katika zoezi la kushtukiza la  ukamataji wa  bidhaa hizo katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam zilizoingizwa nchini kinyume na sheria, kulia ni Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo.


Serikali imefanikwa kukamata jumla ya  bidhaa za filamu na muziki 94,000 ambapo 93,529 ni za wasanii wa nje zilizoingia nchini kinyume na sheria huku bidhaa 273 za wasanii wa ndani zikiwa hazina stampu ya ushuru wa bidhaa kutoka Taasisi ya Mapato Tanzania(TRA) zikiwa ni takwimu za awali.

Hayo yamejiri kufuatia zoezi la kushtukiza lililofanywa na Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye  leo katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuahidi  kwamba zoezi hilo litafanyika nchi nzima.

Aidha aliongeza kuwa mpaka sasa takribani  maduka 42 yamekaguliwa na kukamata  mitambo 19 ya kufyatua kazi za wasanii (duplicators),printer 8 za Cd/Dvd,dvd writers 31,komputa 3,ups 7 kutoka kampuni ya Aguster.

“Hatua hii ni ya mwanzo kwa kuwaonyesha Watanzania kuwa agizo la Rais wa awamu ya Tano Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli la kulipa kodi na kununua bidhaa halisi kwa kutoa risiti linasimamiwa ipasavyo”, alisema Mhe. Nnauye.

Mhe.Nnauye aliongeza kuwa wauzaji wengi wa bidhaa za filamu na muziki wamekiuka sheria  zinazosimamiwa na tasnia ya Filamu na muziki ikiwemo sheria ya Filamu na Michezo ya kuigiza na.4 ya mwka 1976 inayosimamiwa na Bodi ya Filamu Tanzania.

Waziri alizitaja sheria nyingine kuwa ni sheria ya Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na.23 ya mwaka 1984, Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki  na.7 ya mwaka 1999 inayosimamiwa na Chama cha Hakimiliki na Hakishiriki ( COSOTA) pamoja na sheria ya Ushuru wa Bidhaa sura ya 147 chini ya kanuni za stampu kwa bidhaa za Filamu na Muziki ya mwaka 2013 inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA).

Alifafanua kuwa uchumi wa nchi na wasanii umehujumiwa sana kufuatia kuwepo kwa bidhaa za filamu zinazoingizwa nchini na kuuzwa kwa bei nafuu na kuua soko la bidhaa za ndani na kuingiza tamaduni zisizofaa katika jamii na hivyo kuchochea vitendo viovu ikiwemo ushoga.

“Bidhaa nyingi za filamu zimekuwa zikiingia nchini kwa magendo bila kulipiwa kodi na zimekuwa zikuuzwa kwa bei nafuu na hivyo kudidimiza kazi za wazawa na kuikosesha Serikali mabilioni ya fedha kupitia kodi” alisema Mhe.Nnauye.

Waziri Nnauye alitoa wito kwa Watanzania kuwa na tabia ya uzalendo kwa  kukunua bidhaa za filamu zenye stampu ya TRA  ili kusaidia katika kukusanya kodi na kuinua kipato cha wasanii.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Bw. George Haule amewaomba wananchi waunge mkono jitihada za Serikali kwa kununua bidhaa za filamu  zenye stampu ya TRA ili kusaidia kuongeza pato la kodi na kukomesha wale wote wanaokwepa kulipa kodi.

0 Responses to “VIDEO:WAZIRI NAPE AFANYA MSAKO WA FILAMU ZISIZO NA STIKA ZA TRA KARIAKOO ”

Post a Comment

More to Read