Monday, October 10, 2016

TAARIFA YA KIAFYA YA ALIEKUWA MEYA WA JIJI LA DAR ES SALAAM





Aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dkt. Didas Masaburi, amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Masaburi amelazwa hospitalini hapo akipatiwa matibabu, ambayo hata hivyo haijawekwa wazi anasumbuliwa na maradhi gani.

Mmoja wa madaktari wa kitengo cha dharura hospitalini hapo alithibitisha kupokewa kwa kiongozi huyo na kwamba amelazwa katika wodi ya Mwaisela.
 
“Ni kweli Dkt. Masaburi amelazwa hapa Muhimbili wodi ya Mwaisela lakini nakushauri watafute wasemaji au muuguzi wa zamu hao watakupa maelezo zaidi,” alisema.

Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe alikiri kulazwa kwa mwanasiasa huyo.
“Ni kweli amelazwa hapa hospitalini kwa matibabu lakini sina ruhusa ya kukueleza kwanini amelazwa hapa watafute wasemaji,” alisema.

Ofisa Uhusiano wa hospitali hiyo, Neema Mwangomo alipoulizwa kuhusu kulazwa kwa Masaburi alisema hiyo ni siri ya mgonjwa na watu wake wa karibu.
 
“Kiongozi au mtu yeyote akilazwa hapa hatuna ruhusa ya kueleza umma pengine hadi mwenyewe aridhie ni haki yake ya msingi, hatuna mamlaka ya kutoa siri ya mgonjwa,” alisema.
Dkt. Didas Masaburi alikuwa meya wa jiji la Dar es Salaam wakati wa Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
 
Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, aligombea ubunge Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), lakini aliangushwa na Saed Kubenea wa CHADEMA. – MTANZANIA

0 Responses to “TAARIFA YA KIAFYA YA ALIEKUWA MEYA WA JIJI LA DAR ES SALAAM”

Post a Comment

More to Read