Monday, October 24, 2016

WAZIRI MAKAMBA ATOA SIKU TANO KUSITISHWA KWA SHUGHULI ZA KILIMO NA UFUGAJI KATIKA KINGO ZA MTO RUKWA.





Waziri wa Mazingira na Muungano, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe January Makamba  amesema serikali itatangaza eneo la Ziwa Rukwa kuwa eneo nyeti la Mazingira na kuagiza kusitishwa kwa shughuli zote za Kilimo na Ufugaji zinazofanyika katika kingo za Ziwa Rukwa na kutoa siku 5 hadi tarehe 28 mwezi huu kuhakikisha agizo hilo limetekelezwa.

Waziri Makamba ametoa tamko hilo wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Nankanga, Wilaya ya Sumbawanga, Mkoa wa Rukwa  eneo la Forodhani lililopo katika fukwe za Ziwa Rukwa ambapo ametanabaisha kuwa kina cha Ziwa hilo limepungua kwa takribani mita 3 katika kipindi cha miaka 16 ambapo mwaka 2000 kina hicho kilikuwa mita 6 na hivi sasa ni takribani mita 3 pekee.

Waziri Makamba ameainisha kuwa Serikali itachukua hatua za muda mrefu kuokoa Ziwa hilo lakini katika hatua za awali za kuokoa Ziwa Rukwa  ameagiza kuwa kuanzia tarehe 28 ya mwezi huu haitoruhusiwa kufanya Kilimo ndani ya Mita 60 za ukingo wa Ziwa kama inavyotakiwa na Sheria ya Mazingira, Sheria ya Maji na Sheria ndogo za Serikali za Mitaa lakini vilevile kuanzia tarehe 28 mwezi huu haitoruhusiwa kuchunga na kufuga mifugo ndani ya mita 200 za ukingo wa Ziwa.



Katika hatua nyingine Waziri Makamba amesema Serikali itatoa agizo kwa Halmashauri zote za Wilaya ambazo Ziwa Rukwa linapita kukutana na kukusanya pesa kutoka katika vyanzo vyake ili ziweke alama (Beacon) na vibao katika mita 60 na Mita 200 kutoka kwenye Ziwa kujulisha umma kuwa hairuhusiwi kufanya shughuli katika maeneo husika.

Amesisitiza upandaji miti katika mkoa wa Rukwa akisema Mkoa huu bado upo nyuma sana katika upandaji wa miti huku ukataji wa miti ya asili ukiwa ni mkubwa sana hivyo kuagiza zoezi la upandaji miti kuanza mara moja.
Katika kushughulikia tatizo la uvuvi kwa kutumia sumu na baruti amesema serikali itaongeza adhabu ya wote watakaopatikana na kosa hilo ili kukomesha tabia hiyo mara moja

Vilevile ameutaka uongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri kuanza mara moja mchakato wa kujua na kutambua idadi ya mifugo na wamiliki wake ili kuwezesha kutambua eneo sahihi la kutengwa kwaajili ya wafugaji na kupunguza ufugaji holela ambapo hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mifugo namba 12.

Waziri Makamba anaendelea na ziara yake mahsusi ya mazingira katika Mikoa 10 ambapo amepokea taarifa ya Halmashauri ya Mazingira na Misitu ya Wilaya ya Sumbawanga ambayo mbali na mengine imeonesha kuwa imeshatoa notisi kwa wavuvi wanaotumia  zana haramu kwa uvuvi kuzisalimisha zana hizo kwa hiari hadi Novemba 17 na baada ya hapo mamlaka husika na vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki


0 Responses to “WAZIRI MAKAMBA ATOA SIKU TANO KUSITISHWA KWA SHUGHULI ZA KILIMO NA UFUGAJI KATIKA KINGO ZA MTO RUKWA.”

Post a Comment

More to Read