Thursday, February 23, 2017

MKUU WA WILAYA AWACHARAZA VIBOKO WANAFUNZI WA KIDATO CHA SITA


fimbo

Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Odunga amewachapa viboko wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msakwalo walioandamana usiku wa manane kwenda ofisini kwake kudai huduma ya maji, muuguzi na kurejeshewa kwa ratiba ya kula nyama shuleni.
Odunga alisema tukio hilo limesababishwa na utoto wa wanafunzi hao na alilimaliza baada ya kwenda shuleni hapo kuzungumza nao. “Waliomba msamaha na kukiri kutenda kosa ili kurejesha hali ya utulivu, niliamua kuchukua hatua za kinidhamu kwa kuwachapa bakora na wakaendelea na masomo. Wanaendelea vizuri, sijapata tena malalamiko,” alisema.
Taarifa za uongozi wa shule hiyo zinasema kuwa wanafunzi hao wa kidato cha sita waliandamana saa nane usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kwenda ofisi ya Mkuu wa Wilaya, umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka shuleni hapo baada ya kutoroka na walikamatwa wakiwa wameshatembea kilomita 25.
Mkuu wa Shule hiyo, Omary Msemu alisema, “Mkuu wa Wilaya aliwachapa bakora wanafunzi saba, kati yao watano walikuwa ndio vinara wa maandamano hayo na wawili walionesha utovu wa nidhamu wakati alipozungumza nao. Siku moja kabla ya tukio alikuja Afisa Elimu Wilaya kuwaeleza hatua zilizochukuliwa dhidi ya madai yao lakini waligoma kukutana naye na badala yake siku iliyofuata waliandamana.”

Msemu alisema wanafunzi hao waliadhibiwa siku ya Jumamosi kutokana na utoro uliosababisha walimu na walezi kuhangaika kuwatafuta.

0 Responses to “MKUU WA WILAYA AWACHARAZA VIBOKO WANAFUNZI WA KIDATO CHA SITA”

Post a Comment

More to Read