Thursday, February 23, 2017

WANUNUZI WA VITU VYA WIZI NA WANAOFICHA KUKAMATWA


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, Ally Hapi ameagiza Jeshi la Polisi kukamata watu watakaobainika kununua na au kukutwa na vitu vya wizi kwa ajili ya kufanyiwa mahojiano ili waeleze walio wauzia kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Hapi alitoa maagizo hayo Februari 22, 2017 katika mkutano wake na wananchi wa Kata ya Kinondoni, baada ya  wananchi hao kulalamika kuhusu ongezeko la vijana wanao iba kwa kutumia silaha za jadi ikiwemo mapanga.
Licha ya kutoa agizo hilo, aliwataka wazazi na walezi wenye watoto wanaotuhumiwa kwa wizi wa silaha kujisalimisha katika vituo vya polisi vilivyo karibu nao.
“Natuma salamu kwa vibaka wote kuwa hatuna msalia mtume nao, iwe mtoto wa mjumbe au mwenyekiti atakamatwa tu. Kama mzazi unajua mwanao ni mkabaji jisalimishe mapema, na nyumba itakayokutwa na vitu vya wizi mhusika akamatwe,” alisema.
Katika hatua nyingine, Hapi aliagiza watendaji wa kata kuhakikisha mitaa ya kata zao inakuwa na vikundi halali vya ulinzi shirikishi.
Aidha, aliagiza jeshi la polisi kukamata  wamiliki wa vibanda vya bahati nasibu ‘Betting’ wanaoruhusu watoto wadogo kucheza kamali katika vibanda hivyo.

“Polisi andaeni operesheni maalumu ya kupita katika vibanda vya bahati nasibu, mkiwakuta watoto kamateni wamiliki wa vibanda husika weka ndani au mamlaka husika ziwanyang’anye leseni,” alisema.

0 Responses to “WANUNUZI WA VITU VYA WIZI NA WANAOFICHA KUKAMATWA”

Post a Comment

More to Read