Thursday, February 23, 2017

MVUA YASABABISHA MAAFA,YAHARIBU NYUMBA ZA TAASISI


Mvua iliyoambatana na upepo wa kimbunga, umesababisha majanga kwa wakazi wa kijiji cha Mtera wilayani Mpwapwa mkoa wa Dodoma, baada ya nyumba 93 na taasisi tano kuharibiwa zikiwamo shule mbili na kanisa.
Picha: Maktaba
Akizungumza kwa njia ya simu leo akiwa njiani kuelekea sehemu ya tukio, Mkuu wa wilaya hiyo, Jabir Shekimweri, amesema mvua hiyo iliyonyesha juzi mchana katika kijiji cha Mtera, ilisababisha maafa hayo kwa wakazi wa kijiji hicho.
“Ni kweli mvua imesababisha madhara katika kijiji hicho kwa kuezua nyumba 93 yakiwamo majengo mawili ya taasisi za serikali, makanisa matatu na kujeruhiwa na watu watatu,” amesema Shekimweri.
Shekimweri amesema katika nyumba hizo zilizoharibiwa na kimbunga hicho, 40 zimeezuliwa kabisa, 41 zimeezuliwa nusu ya nyumba huku nyumba 12 zikiwa zimeondolewa kati ya bati mbili na tano.

Jabir Shekimweri - DC Mtera
Amesema kati ya watu watatu waliojeruhiwa kutokana na athari hiyo na kukimbizwa hospitalini, wawili waliruhusiwa baada ya kufanyiwa matibabu na mmoja bado anaendelea kutibiwa kutokana na kuvunjika mguu.
Sehemu mbalimbali ya mkoa wa Dodoma, mvua iliyodumu kwa saa nne ilinyesha jana kuanzia saa 3:30 asubuhi hadi saa 8 mchana, hivyo kusababisha madhara katika baadhi ya maeneo.

0 Responses to “MVUA YASABABISHA MAAFA,YAHARIBU NYUMBA ZA TAASISI ”

Post a Comment

More to Read